Menu
 

Habari na Rashid Mkwinda, Mbeya.
Kikao cha kamati ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ileje mkoani Mbeya kimepitisha maamuzi ya kuwasimamisha kazi watumishi wanne wa halmashauri hiyo waliotuhumiwa katika jaribio la wizi wa sh milioni 86.2 zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hewa katika kata ya Ruswisi na Ibaba wilayani humo.

Akitangaza maazimio ya kamati ya madiwani iliyoketi kujadili tuhuma za watumishi hao Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw. Mohamed Mwala amewataja watumishi waliosimamishwa kupisha sheria kuchukua mkondo wake kuwa ni Bi. Subilaga Kapange ambaye kaimu mweka hazina wa wilaya hiyo na watumishi wengine watatu.

Bw. Mwala amewataja watumishi wengine kuwa ni Ofisa Mipango  wa wilaya hiyo Bw.Mchuuzi Limbanga,Bw.Henry Kagogoro ambaye ni Ofisa Utumishi na Bw. Anyitike Chisunga ambaye ni mhasibu msaidizi wa wilaya.

Awali kabla ya kupitishwa kwa uamuzi huo kubadili kikao cha baraza kuwa kamati kuliibuka majadiliano ya kuzuia kuwepo kwa kikao hicho ambapo Mwanasheria wa halmashauri Bw.Agape Fue alidai kwamba kwa kuwa suala hilo lipo katika upelelezi wa polisi si vyema madiwani wakaliwekea mjadala. 

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ibaba Bw. Tata Kibona amesema kuwa suala hilo linapaswa kujadiliwa katika kamati ili kuweka uwazi juu ya tuhuma zilizopo kwa watumishi hao na kwamba kitendo cha kuendelea kuficha ukweli kitaendelea kuficha ukweli juu ya tuhuma za watumishi hao ambao hadi sasa wanaendelea kuripoti kazini.

Naye Diwani wa kata ya Ruswisi Bw. Rauden Tuya amesema bila kuweka mkazo juu ya suala hilo kuna hatari ya halmashauri hiyo kupata hati chafu, hivyo ni vyema kuwekea mkazo wa kuwawajibisha watumishi wenye nia mbaya na halmashauri hiyo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bi. Sylivia Siriwa amesema kuwa mara baada ya kupata taarifa za jaribio hilo aliwasiliana na Meneja wa Benki ya NMB kusimamisha ulipaji wa fedha hizo kwa kuwa hakuna mradi wa aina hiyo katika kata za Ruswisi na Ibaba na  baadaye aliwaonya kwa kuwandikia barua watumishi hao.

Post a Comment

 
Top