Menu
 

Habari na Rashid Mkwinda, Mbeya.
Wanawake waishio wilaya ya Ileje, Mkoani Mbeya wametakiwa kuachana na dhana potofu za kuwaficha watoto wenye ulemavu na badala yake wametakiwa kujitokeza na watoto hao Agosti 26, mwaka huu kwa ajili ya sensa ya watu na makazi ambayo itaendeshwa nchini kote.

Zoezi hilo la sensa limelenga kuhesabu watu ili kupata takwimu sahihi ya wakazi kwa nia ya kuiwezesha serikali kujua idadi ya watu kwa lengo la kupanga mikakati ya maendeleo kutokana na idadi kamili ya wananchi.

Akizungumza katika zoezi la uhamasishaji wa sensa wilayani humo Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Mbeya Bi. Hilda Ngoye amesema kuwa kumekuwepo na desturi ya wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu na kuwataka kuwafichua wakati wa sensa ya watu na makazi.

Amesema kuwa wapo baadhi ya wakazi wa maeneo ya vijijini ambao wamepandikizwa itikadi kuwa zoezi la kuhesabu watu lina nia  ya kupunguza watu kwa kuwafunga vizazi akina mama na kwamba si kweli bali serikali inahitaji kuweka mipango juu ya takwimu sahihi za wakazi wake ili kupanga maendeleo.

Pia amewataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao wakati wa uboreshaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kwamba mawazo ya wananchi yatakayotolewa yatasaidia kuunda Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya Watanzania katika mfumo wa kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Akizungumzia mikakati ya wanawake kujikwamua kiuchumi Bi. Ngoye amesema kuwa wanawake wanayo fursa kubwa ya kujiwezesha kwa kubuni kazi za mikono ikiwemo ufugaji, ususi na ufinyazi na kwamba ili kuweka uwiano wa kiuchumi katika jamii wanawake wanatakiwa kuacha utegemezi na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali.

Amebainisha kuwa zipo fursa nyingi kwa akina mama ambazo zikitumiwa ipasavyo wanawake wanaweza kujikwamua kiuchumi na kuongeza kuwa wanawake waishio maeneo ya mipakani wanazo fursa za kipekee kwa kutumia rasilimali za hapa nchini na kuwauzia nchi jirani za Zambia na Malawi.

Hata hivyo Bi. Ngoye amekutana na Vikundi saba vyenye jumla ya akina mama 210 katika kata za Mawindi, Rujewa, Mswiswi, Chimala vilivyopo katika wilaya ya Mbarali, Itumba iliyopo katika wilaya ya Ileje, Kyimo iliyopo katika wilaya ya Rungwe na Lisungo iliyopo katika kata ya Kyela.

Post a Comment

 
Top