Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga,Rungwe.
Bibi mmoja(Ajuza) Mkazi wa Kijiji cha Kilasi,Kata ya Luteba,Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya Bi.Bestauni Kagenda(60), amejeruhiwa vibaya baada ya kuvamiwa na bundi wapatao 8 alipoingia nyumbani kwake wakati akitokea kuteka maji mtoni.

Bibi huyo alikubwa na mkasa huo baada ya kufungua mlango majira ya saa 12:00 jioni Mei 30 mwaka huu na kukutana na kundi la bundi hao, ambapo walianza kumvamia sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali.

Aidha Bi Kagenda amesema wakati akitoka kuelekea kuyateka maji mtoni alikuta bunti hao wameketi eneo la makazi yake na walipomuona walianza kumshambulia mwilini.

Hata hivyo tukio hilo limearifiwa kwa Mzee wa Kimila,ambapo waliitisha mkutano wa hadhara na kuonya juu ya vitendo vya kishirikina na kupinga maovu yote yanayotokea katika jamii hiyo.

Wakati huohuo Chifu wa Kinyakyusa Bwana Angasisye Asani amewataka wakazi wa eneo hilo kuachana na mila potofu, hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa wakazi wa kijiji hicho.

Naye Mwenyekiti wa kijiji Bwana Asangalwisye Kahole amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba anawaachia wazee wa mila ili wabaini tatizo linalowakabili.

Mbali na tukio hilo umezuka ugonjwa wa ajabu wa kuwashwa mwili mzima unaoambatana na upele kwa wanafunzi na baadhi ya wakazi wa Kijiji hicho cha Kilasi.

Akiongea kwa masikitiko makubwa Mwenyekiti huyo Bwana Kahole amesema tangu ugonjwa huo uvamie kijijini hapo ni juma moja sasa ambapo wanafunzi wa shule mbalimbali kijijini hapo hawaendi shule kutokana na adha ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rungwe hakupatikana kuzungumzia suala hilo.   

Post a Comment

 
Top