Menu
 

Habari na Angelica Sullusi,Mbeya.
Sakata la Mgomo wa Madaktari limeingia katika sura mpya Mkoani Mbeya baada ya Bodi ya Hospitali ya Rufaa Mbeya ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kutishia kusitisha mikataba ya madaktari waliogoma hasa wale ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Norman Sigalla amewaambia waandishi wa habari leo kuwa Bodi imefikia uamuzi huo baada ya kuona  madaktari hao wamevunja mkataba wao na hospitali hiyo ambao unawataka kufanya kazi bila kugoma.

Aidha, amesema kabla ya kuwaandikia barua hiyo, juzi bodi ya Hospitali ilikutana na kuwaita madaktari wote kwa barua ili wakae nao na kuwasikiliza madai yao lakini hakuna daktari hata mmoja aliyejitokeza kwenye kikao hicho.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa sheria za kazi mtumishi asipofika kazini kwa muda wa siku tato mfululizo anakuwa amejifuta kazi mwenyewe, hivyo kama madaktari hao hawataripoti kazini kufikia leo, watalazimika kuwaondoa na kuwarejesha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye aliwatuma kwenda kufanya mazoezi ya vitendo hospitalini hapo.

Akizungumzia madaktari waliosajiliwa ambao wanashiriki mgomo huo, Dk. Sigalla amesema  na wao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye mwajiri wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky amezungumzia madhara yaliyosababishwa na mgomo huo kwa wagonjwa, kuwa tangu madaktari hao kugoma kuwa wagonjwa waliofika hospitalini hapo kwa matibabu wameathirika kwa namna moja ama nyingine kwa kuwa hakukuwa na huduma ya kuridhisha.

Post a Comment

 
Top