Menu
 

Mwandishi wa Kampuni ya Business Times inayochapisha gazeti la MAJIRA mwakilishi wa mkoa wa Mbeya Bw. Charles Mwakipesile amekuwa ni miongoni mwa wagombea 24 waliojitokeza kuchukua fomu katika ofisi ya CCM wilaya ya Mbeya mjini kuwania nafasi za Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa  CCM Taifa.

Bw. Mwakipesile ambaye alikuwa ameambatana na Katibu mwenezi wa CCM Kata ya Itiji Bw. Livingstone Mwakapesa na Katibu wa CCM kata ya Mwakibete Bw.George Mapunda amerudisha fomu hiyo mbele ya Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya Bw.Raymond Mwangwala na kusema kuwa ameamua kujitosa katika siasa kuleta changamoto kwa vijana.

Amesema kuwa CCM ni chama kikongwe ambacho kikipata viongozi vijana kinaweza kurekebisha dosari ndogondogo zinazojitokeza ambazo ni changamoto zinazotokana na kukua kwa demokrasia ya vyama vingi nchini.

Amesema ili kukabiliana na changamoto chama kinahitaji kuwa na nguvu kubwa ya vijana ambao anaamini kwa kushirikiana na busara za wazee kinaweza kupiga hatua hasa kutokana na historia yake ya kuongoza kwa amani, utulivu kwa zaidi ya miaka 40.

Akizungumza wakati akipokea fomu hiyo Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya Bw.Mwangwala amesema kuwa amefurahi kuona vijana wamejitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kwamba hadi sasa jumla ya wanachama 24 wamejitokeza kuchukua fomu na kurejesha jana mchana.

Bw. Mwangwala amesema kuwa kila mwanachama anayo haki ya msingi kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwa nia ya kuleta changamoto ndani na nje ya chama.

Post a Comment

 
Top