Menu
 

 
Baadhi ya dawa zilizotelekezwa na wauguzi baada ya kukiacha kituo cha kazi,siku nne baada ya mwenge wa uhuru kukizindua kituo hicho(Picha na Ezekiel Kamanga).. 

*Dawa zakabidhiwa kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kijiji.
*Wanawake wawili ambao ni wajawazito wajifungulia njiani.
 ******
Habari na Ezekiel Kamanga,Chunya.
Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kuhakikisha huduma za kijamii zinasogezwa jirani zaidi na makazi ya watu,Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mpona,Kata ya Totowe,Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,kimeachwa bila watumishi baada ya waliokuwa wamefikishwa kutoweka hali iliyochangia akina mama wawili wajawazito kujifungulia njiani.

Kituo hicho kimeachwa mikononi mwa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bwana Bahati Mwanguku na Mwenyekiti wake Bwana Nestory Mwashadewa.

Kittuo hicho cha Afya kilizinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Kepteni Honest Ernest Mwanossa,Mei 12 mwaka huu ambapo watumishi wawili wa afya walipelekwa kwa ajili ya kutoa huduma ambao ni Tabibu,msaidizi Bwana Manase Sinkamba na Muuguzi msaidizi Bi F. Mwaisakilaambao walitipoti kituoni hapo Mei 10 na kuanza kutoa huduma kwa wakazi wa kijiji hicho Mei 11 mwaka huu.

Aidha kituo hicho kilifunguliwa kwa furaha kubwa kutoka kwa wananchi wakati wa mbio za Mwenge wa uhuru,wakiamini kuwa ni ukombozi na changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwa sekta ya afya zimeisha.

Katika hali ya kushangaza wahudumu hao walitoka  kituoni Mei 16 mwaka huu wakidai kuwa wao waliazimwa tu kwa muda na kwamba walipewa siku 4 za kutoa huduma katika kijiji hicho hivyo hadi sasa kituo hicho hakifanyiwi kazi kufuatia adha kubwa kwa wananchi zaidi ya 2000,ambao walijenga kituo hicho kwa jitihada kubwa ambapo kiligharimu zaidi ya shilingi milioni 4.

Wananchi wameiomba Serikali kufanya haraka iwezekanavyo kuwaleta wahudummu wengi,ambapo akina mama wajawazito kujifungulia njiani kutokana na kusafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 8 kwani baadhi yao wamekuwa wakipanda mikokoteni na wengine kutembea kwa miguu.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chunya amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba si muda mrefu waganga wa kituo hicho watapelekwa kijijini humo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Bwana Deodatus Kinawiro,amekiri kupokea taarifa za tatizo hilo ingawa amewataka viongozi wa kijiji hicho kuwasilisha malalamiko yao rasmi kwa barua ili aweze kuchukua hatua za haraka kukabiliana na adha hiyo kwa wananchi.

Kituo hicho cha afya mbali na kutoa huduma kwa wakazi wa kijiji hicho,ilikuwa isaidie vijiji vya jirani kutokana na Jografia ya wilaya hiyo kuzungukwa na makabila ya Maasai,Wasukuma na Wamang'ati ambao wamehamia wakiwa na mifugo.

Post a Comment

 
Top