Menu
 

Sudan mafuta Mawaziri wa ulinzi kutoka Sudan na Sudan Kusini wanaendelea na kikao maalum mjini Addis Ababa, Ethiopia, kujadili masuala ya ulinzi na usalama mipakani mwao kutokana na kuibuka kwa migogoro.

Pagan Amun ni mjumbe wa kutoka serikali ya Sudan Kusini aliyepo Addis Ababa, na hapa anazungumzia madhumuni la mkutano huo. " Mkutano wetu unatupia jicho kuwepo utaratibu wa kuweka mikakati ya usimamizi wa mipaka baina ya nchi zetu mbili, pia kuunda kamati ya kupokea malalamiko ya pande zote mbili kama kukiwa na upande mmoja umekiuka makubalino ya mipaka yaliyofikiwa."

Mkutano huu, ukibarikiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, AU, umeanza jana, huku wajumbe kutoka pande zote na viongozi wakuu wakikutana ili kuepusha kutokea kwa mapigano ya mpakani kwenye maeneo yanayogombaniwa, ambapo utata juu ya mipaka ya sasa na ile ya zamani likiwa tatizo kubwa.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wamezipa Sudan muda wa miezi miwili, hadi Agosti 2, ziwe zimeshapata suluhu juu ya mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuainisha mpaka wa kila moja, usafirishaji wa mafuta na masuala ya uraia.
Mazungumzo yanafanyika bila masharti

Mjumbe Amun ameongeza kuwa pande husika na jopo la mazungumzo wamekubali kutekeleza kikamilifu azimio namba 2046 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mpango wa Umoja wa Afrika.

"Tumekubaliana kuzungumza bila ya kuwa na masharti yoyote yale, pia Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika kwa pamoja wametuomba tufanye hivyo." Alisema Mjumbe huyo

Mjumbe huyo kutoka Sudan Kusini alisema kuwa jopo la usuluhishi la Umoja wa Afrika liliitisha mkutano tarehe 7 Juni kujadili juu ya jimbo la Abyei ambalo limekuwa chanzo kikuu cha uhasama baina ya Sudan na Sudan Kusini. Anasema pande mbili zinajadili juu ya kuanzishwa utawala na mifumo mingine muhimu ya kurejesha amani jimboni humo.

Mazungumzo haya yalitanguliwa na shutuma wiki iliyopita, Sudan Kusini ikiishtumu Sudan kwa kukataa kuondoa majeshi yake kutoka Abyei. Umoja wa Mataifa ulikuwa umezipa nchi hizo hadi Mei 16 kuondoa majeshi yao kutoka Abyei, lakini Sudan haikuondoa majeshi yake hadi tarehe Mosi Juni.

Sudan na Sudan Kusini zilipigana vita kwa muda mrefu na mwaka jana Sudan Kusini ikapata uhuru wake na kuwa taifa huru, lakini mwaka huu nchi hizo mbili ziliingia katika mapigano mara baada ya Sudan Kusini kuuteka Mji wenye utajiri wa mafuta wa Heglig, na baadae Sudan kuwafurusha askari walikuwepo katika mji huo na kusababisha vifo vya askari wengi katika mapigano hayo.

Mwandishi:Adeladius Makwega/RTRE
Mhariri: Miraji Othman

Post a Comment

 
Top