Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mwanafunzi wa Kidato cha nne,shule ya sekondari Nyerere,iliyopo Mji mdogo wa Tunduma,Wilaya ya Momba,Mkoani Mbeya Boaz Mwalusanya(18) amefariki dunia baada ya kujinyonga.

Tukio hilo limetokea baada ya ugomvi uliokuwepo shuleni hapo,mapema majira ya saa mbili asubuhi Juni 5 mwaka huu,kabla ya mkutano wa wazazi uliotakiwa uanze majira ya saa 5 asubuhi siku hiyo hiyo.

Diwani wa Kata ya Tunduma Mheshimiwa Frank Mwakajoka,amesema marehemu alijinyonga baada ya kutumiwa kuwa ni miongoni mwa wanafunzi walioanzisha vurugu,zilizopelekea ugomvi mkubwa uliohusishwa na silaha za visu,hivyo kusababisha majeraha kwa baadhi ya wanafunzi.

Katika vurugu hizo baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walitorokea Wilaya ya Nakonde nchi jirani ya Zambia.

Miongoni mwa wanafunzi waliojeruhiwa na visu ni pamoja na Abel Ndihesya(17) na Asifiwe Kiungulia(16) wote ni wanafunzi wa kidato cha nne,ambapo walikimbilia katika Kituo cha Afya cha Tunduma  na hali zao zinaendelea vizuri.

Chanzo cha ugomvi baina ya wanafunzi shuleni hapo hakijaweza kufahamika,ambapo Walimu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanafanya uchunguzi ili kubaini hali iliyosababisha mchafuko shuleni hapo.

Aidha Jeshi hilo lina mshikilia mwanafunzi mmoja Mloli(19),anayesoma kidato cha nne katika shule hizo kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo mheshimiwa Mwakajoka,amewataka wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo kukutana mapema haraka iwezekanavyo ili kurejesha amani shuleni hapo.

Miongozi mwa sababu za magomvi shuleni hapo baina ya wanafunzi ilitokana na baadhi yao kudaiwa wanatumia vileo na uvutaji wa bangi hali inayosababisha kutokuwepo kwa usikivu kwa walimu na kuleta vurugu kwa wanafunzi wenzao na pindi wanapokatazwa kuwatishia.

Mgogoro umedumu shuleni hapo kwa siku kadhaa na imechangia walimu na wanafunzi kutopatikana na kudhorotesha mfumo mzima wa uwajibikaji kwao.

Post a Comment

 
Top