Menu
 

Wavuvi wadogo watano kati yao watatu wa familia moja na askari mgambo wawili wameuawa na mwanafunzi kunusurika, baada ya kupigwa hadi kufa na kisha kuchomwa moto na watu wanaodaiwa kuwa wavuvi wakubwa katika kisiwa cha Kasalazi, kijiji cha Lushamba, Ziwa Victoria, wilayani Sengerema.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana, baada ya watu wanaodaiwa kuwa wavuvi wakubwa kuwateka ziwani na kisha kuwapeleka nchi kavu, wakiwawatuhumu kuwa wavuvi haramu na wezi wa nyavu.

Taarifa zinaeleza kwamba, hali hiyo ilitokea baada ya kutokea mtafaruku kati yao ziwani, majira ya saa mbili usiku.

Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Lushamba, aliyenusurika na aliyejitambulisha kwa jina la Defao Zacharia Ombajo (17), alisema mauajia hayo yalifanyika saa tano usiku, umbali wa zaidi ya kilometa moja kutoka nchi kavu baada ya kukutana na wavuvi wakubwa.

Alisema wao walikuwa kwenye mtumbwi mdogo usiokuwa na namba za usajili, lakini mara wakatokea wavuvi wakubwa wakiwa na mtumbwi ulioandikwa ubavuni Mv. Msimbazi ambao waliwaamuru kuondoka ziwani.

Defao alieleza kuwa, walikaidi amri ya  wavuvi hao wakubwa, ndipo walipoanza kurushiwa mawe na wavuvi hivyo walilazimika kupiga kelele kuomba msaada.

''Hata hivyo, tulipoanza kupiga kelele kutafuta msaada, wao waliwaita kwa simu wenzao ambao walifika eneo la tukio wakiwa na mitumbwi zaidi ya mitano na kutuzingira na kisha kuanza kutupeleka nchi kavu katika kisiwa cha Kasalazi wakiwa tayari wamekwisha kutushambilia na baadhi yetu kujeruhiwa vibaya…walituzidi nguvu,'' alidai Defao.

Alifafanua kuwa wakiwa chini ya ulinzi, kaka yake aitwaye Dismas alimpigia simu baba yao Zacharaia Ombajo ambaye alikwenda na wazee wawili, Hamis Msafiri na Jumanne Eavarist lakini nao waliwekwa chini ya ulinzi na baadaye kuuwa na kuchomwa moto pamoja.

Alisema kuwa yeye, kaka yake na Richard Magori ambaye ni baba yake mdogo walikwenda ziwani kwa lengo la kuvua.

Alizungumza kwa majonzi, alisema matokeo yake baba yake mzazi, baba yake mdogo na kaka yake waliuawa na kuchomwa moto.

“Walipotufikisha nchi kavu pale Kasalazi nilifanikiwa kutoroka kwa msaada wa msamaria mwema ambaye simfahamu...lakini niliporudi baadaye nilikuta baba yangu amekufa na akiwaka moto, amechomwa pamoja na wale wengine wanne,” alidai Defao akitokwa machozi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, alithibitisha tukio hilo kutokea, lakini alieleza ufafanuzi ungetolewa baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Sengerema itatakaporejea kutoka eneo la tukio.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lushamba, Ezekiel Galula, akithibitisha kuwepo kwa atukio hilo na amewataja waliouawa kuwa ni waliokuwa askari mgambo wa kijiji hicho, Richard Magori na Mzee Hamis Msafiri, Zacharia Ombajo, Jumanne Evairist na Dismas Ombajo.

Alisema Zacharia, Richard na Dismas ni wafamilia moja na kusisistiza kuwa mauaji hayo ni ya kikatili na yanastahili kuchukuliwa hatua kali kwa lengo la kuyakomesha.

Alisema wananachi wameyapinga na kueleza kuwa waliouawa hawana rekodi ya wizi wa nyavu ziwani japokuwa siku chache kabla ya tukio hilo, wavuvi wa kambi ya Msimbazi walidai kuibiwa injini yao na watu wasiojulikana.

Mwenyekiti huyo alilaani kitendo hicho na kudai kuwa, baadhi ya waliouawa walikuwa wamekwenda kutoa msaada akiwemo baba mzazi wa kijana Defao.

Baadhi ya wananchi akiwemo Gelard Khan (46), wametahadharisha kuwa endapo hatua kali hazitachukuliwa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka mapambano makubwa ya kulipiza kisasi.

 HABARI NA RENATUS MASUGULIKO
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top