Menu
 

 Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Mwanyanje, Kata ya Igawilo mkoani Mbeya wakiwa na nyuso za huzuni baada ya mwananchi mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja kupigwa na kisha kuchomwa moto na mwili wake kutelekezwa. Mtu huyo aliuwawa kwa tuhuma za wizi wa kitu ambacho mpaka sasa hakijafahamika na muibiwa mwenyewe kuto tambulika.(Picha na maktaba yetu).
*****
Habari na Angelica Sullusi,Mbeya.
Imeelezwa kuwa zaidi ya watu 600 waliuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira kali walioamua kujichukulia sheria mkononi katika kipindi cha mwaka jana pekee. 

Hayo yamesemwa na Wakili na Afisa wa ufuatiliaji wa Haki za Binadamu kutoka katika kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Laetitia Ntagazwa wakati akitoa mada kwenye mafunzo ya waangalizi wa Haki za Binadamu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika Jijini Mbeya. 

Amesema utafiti uliofanywa na LHRC umeonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana pekee watu zaidi ya 600 wameuawa kwa kupigwa na wananchi, hali ambayo inaashiria kuwa vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi vinazidi kukithiri nchini. 

Aidha, Ntagazwa amesema  kufuatia kuongezeka kwa vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na ukiukwaji wa haki za Binadamu, Kituo cha Haki za Binadamu kimeamua kuchukua hatua ya kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za kujichukulia sheria mkononi. 

Amesema miongoni mwa mambo ambayo LHRC kinataka kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi ni kampeni ya utii bila Shuruti, ambapo wameamua kuwashirikisha Polisi kila mahali wanapokwenda kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waangalizi wa haki za binadamu.

Post a Comment

 
Top