Menu
 

Wakati maiti 58 wakiwa wamepatikana, wazamiaji bingwa wa kizalendo wamesema wameshindwa kuiona boti ya Mv Skagit kutokana na kuzama katika kina kirefu cha bahari ya Hindi karibu na kisiwa cha Pungume, Zanzibar.


Wakizungumza na NIPASHE wakitokea eneo la ajali, walisema kwamba maiti zimekuwa zikionekana zikielea baharini, lakini meli wameshindwa kuiona tangu kutokea kwa ajali hiyo juzi.

Hadi majira ya saa 12:00 jioni jana maiti 58 walikuwa wamepatikana, 47 tayari wametambuliwa na ndugu zao na watu 150 wameokolewa likiwemo kundi la watalii 10 kutoka Uholanzi, lakini raia mmoja wa Marekani amekufa katika ajali hiyo.

Mzamiaji Ali Ramadhan, alisema wamejaribu kuzamia umbali wa mita 25 wakitumia mitungi ya hewa ya oxygen lakini wameshindwa kuiona meli hiyo.

Alisema kutokana na meli hiyo kuzama katika kina kirefu uwezekano wa kuopolewa ni mdogo na wanaendelea kutafuta maiti ambazo zimekuwa zikisukumwa na mawimbi ya bahari katika eneo hilo.

“Tumejaribu kuzamia umbali wa mita 25 tumeshindwa kuiona meli ingawa maiti zinaendelea kuonekana baharini,” alisema mzamiaji huyo.

Alisema kwamba matumaini ya meli hiyo kuja juu ni madogo kutokana na kuzama katika mkondo mkubwa wa maji, lakini alisema juhudi za kuwatafuta watu wakiwa hai au wamekufa zinaendelea kufanyika.

Kwa upande wao mabahari walioshiriki katika kazi ya uokoaji, wamesema kwamba pamoja na boti ya Kilimanjaro III kufika mwanzo katika eneo la tukio kazi ya kuopoa maiti ilikuwa ngumu kutokana na ukosefu wa vifaa na mafuta ya kuendeshea boti ndogo iliyokuwemo ndani ya meli hiyo.

Baharia mmoja alisema kwamba boti hiyo iliondoka bila ya kuchukua mafuta na baada ya kufika katika eneo la tukio boti yao kwa kuwa ni kubwa ilichangia kuwasukuma mbali zaidi maiti kutokana na mawimbi makubwa ya maji ya bahari.

Alisema kwamba kazi za uokoaji kama hiyo hutakiwa kutumika boti nyepesi badala ya ya kubwa. Boti ndogo za polisi zilikwama katika bandari ya Malindi na kuondoka majira ya saa 11:15 jioni kutokana na ukosefu wa mafuta tangu kutokea kwa ajali hiyo saa 7:30 mchana juzi.

“Kuna maiti tulikuwa tunaziona zinaelea juu, lakini kwa kuwa boti yetu kubwa ilichagia kuwasukuma kwa mawimbi ya bahari bahati mbaya na hiyo boti yetu ndogo haikuwa na mafuta,” alisema baharia mmoja katika boti ya Kilimanjaro.


Aidha alisema kwamba sehemu kubwa ya watu wamekufa na wengine kupotea kutokana na uzembe wa vyombo vya ulinzi na usalama wa raia kushindwa kufika kwa muda muafaka katika eneo la ajali.


Mahabaria hao walisema kwamba pamoja na boti kuzama katikati ya Dar es Salaam na Zanzibar mawasiliano ya radio yalikuwa yanapatikana baina ya pande hizo mbili, lakini hakuna chombo cha uokoaji kilichofika kutoka Tanzania Bara.

Walisema kwamba badala yake Kikosi cha Jeshi la Polisi cha wanamaji na bandari walifika jana na kuungana na wenzao wa KMKM kufanya kazi ya kutafuta maiti katika eneo la ajali tangu kutokea ajali hiyo juzi majira ya saa 7:30 mchana juzi.

Walisema kwamba boti hizo mbili baada ya kuwasili Zanzibar moja ilipangiwa kwenda katika eneo la ajali na boti nyingine yenye namba 001 Naval Command ilibakia katika bandari ya Malindi kama chombo cha akiba kama viongozi wa Kitaifa watataka kwenda katika eneo la tukio hilo.

ZPC WALAUMIWA
Katika tukio jingine, baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Bandari wamelalamika juu ya kitendo cha Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) kugoma kutoa Sh. milioni moja kusaidia mafuta yaliyokuwa yanahitajika kwa matumizi ya boti za uokoaji.

Walisema kwamba Kaimu Mkurugenzi ZPC, Msanifu Mussa Haji, baada ya kutakiwa kutoa fedha hizo alikuwa mkali na kuwataka wenzake kuzingatia mgawanyo wa majukumu na kusababisha boti tatu kuondoka saa 11:15 kwenda katika eneo la ajali takribani saa nne tangu kutokea kwa ajali hiyo.

Akizungumza na NIPASHE eneo la Malindi Mjini Zanzibar, Haji, alikanusha madai hayo na kusisitiza kwamba wao ndiyo walikuwa wa kwanza kupeleka tangi lao la mafuta baada tu ya kupokea taarifa za kuzama kwa boti hiyo.

Hata hivyo, alisema kwamba suala la Zanzibar kukosekana kikosi maalum cha uokoaji baharini siyo jukumu lake na wanaopaswa kuulizwa ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Zanzibar (ZMA).

Naye Kaimu Mkurugenzi wa ZMA, Abdalla Hussein Kombo, alisema kwamba jukumu la uokoaji ni kazi inayostahili kufanywa mara tu baada ya kupokea taarifa kutoka Kituo cha Uokoaji na Utafutaji Baharini Tanzania (RMCC).

Alisema kwamba kituo hicho ndicho kinapokea taarifa za mwenendo wa hali ya hewa kila siku kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na jukumu lake kubwa ni kufanya kazi za uokoaji katika majanga kama hayo.

BOTI ILITENGENEZWA MAREKANI 
Alisema kwamba boti hiyo ilitengenezwa Marekani ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 380 mwaka 1989.

Ililetwa Zanzibar Oktoba mwaka 2011 na ukaguzi wa mwisho ulifanyika Mei mwaka huu na kuruhusiwa kufanya kazi kwa masharti maalum.

Alisema kwamba, pamoja na chombo hicho kuwa na uwezo wa kuchukua abiria 380, lakini kiliruhusiwa kuchukua abiria mwisho 250 huku kikiwa chini ya uangalizi juu ya kiwango chake cha ubora.

Kombo alisema kwamba baada ya chombo hicho kukaguliwa kilibainika kuwa na viyoyozi vibovu na wahusika walitakiwa kufanya matengenezo kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi.

Alisema kwamba boti hiyo inamilikiwa na Mfanyabiashara Said Abdulraman, na  ilikuwa imebakisha miaka miwili kumaliza muda wake wa matumizi tangu kujengwa kiwandani.

Taarifa zinasema kwamba boti hiyo iliongezwa ghorofa nyingine juu tofauti na ilivyokuwa imetengezwa awali kiwandani kwa malendo ya kuongeza uwezo wa kuchukuwa abiria zaidi, lakini Mkurugenzi wa ZMA alisema wakati meli inasajiliwa yeye hakuwepo katika ofisi hiyo.

Alisema kwamba boti hiyo imesajiliwa kwa ajili ya abiria na hairuhusiwi kuchukua mizigo.

Alisema kwamba boti hiyo ilikuwa na mahaharia tisa akiwemo Nahodha Mussa Makame; Fundi Mkuu, Ibrahim Ali Haji, na msaidizi nahodha wake, Mayasa Mohamed wakazi wa Zanzibar.

NCHIMBI: TUSITAFUTE MCHAWI
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kwamba wakati huu siyo wa kutafutana uchawi badala yake ni wa kufanya kazi ya kuokoa waathirika wa ajali hiyo.

Alisema kwamba serikali itatumia nguvu zake sote kuwatafuta watu ambao bado hawajapatikana na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kufanikisha kazi hiyo.

Alisema vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vinaendelea na kazi ya kutafuta watu ambao bado hawajapatikana kupitia vikosi vya ulinzi na usalama na wananchi.
NAHODHA, MMILIKI WASAKWA
Kamishina wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema kwamba nahodha wa meli hiyo pamoja na mmiliki wake wanatafutwa na polisi na bado hawajapatikana tangu kutokea kwa ajali hiyo.

Hata hivyo, alisema kwamba kuna mabaharia wawili wamefanikiwa kuwapata na tayari wameanza kusaidia uchunguzi, lakini hadi jana alikuwa bado hajapata idadi ya orodha ya abiria waliosafiri na meli hiyo.

Juhudi za NIPASHE kuzungumza na mmiliki wa meli hiyo jana hazikufanikiwa kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita tu bila ya kupokelewa.

WAZIRI: SITAJIUZULU 
Wakati huo huo, wakati wananchi kadhaa katika Manispaa ya Zanzibar wakimtaka Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hama, ajiuzulu, amesema  kwamba hakuna mtu wa kulaumiwa kwa kuwa ajali hiyo ni sawa na majanga mengine kama ya sunami au kimbunga.

Akizungumza na waaandishi wa habari katika uwanja wa kutambua maiti Maisara, Hamad, alisema kwamba hakuna sababu za msingi yeye kujiuzulu kwa vile tukio hilo ni mipango ya mwenyezi Mungu.

 “Sioni sababu ya kujiuzulu tukio hili ni mipango ya mwenyezi mungu kama majanga mengine yanavyotokea kama kimbunga na sunami,” alisema waziri huyo.

Alisema kwamba boti hiyo ilipinduka na kuzama baada ya kupingwa na mawimbi makali baada ya bahari kuchafuta wakati ikitokea Dar es Salaam.


Hata hivyo, baadhi ya wananchi wakizungumzia tukio hilo walisema kutokana na uzembe uliyofanyika katika ukoaji, viongozi na watendaji wakuu wanastahili kuwajibika.


Walisema kwamba tukio hilo limetokea miezi tisa tangu kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 941 lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na wizara hiyo ya  kuimarisha huduma za uokoaji na ukaguzi wa meli Zanzibar.

SMZ KUBEBA GHARAMA
Katika tukio jingine, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kwamba SMZ itasimamia gharama zote za mazishi ya waliofariki pamoja na kutoa huduma ya afya na matibabu kwa majeruhi wote wa ajali hiyo.

Aidha, alisema kwamba sherehe na tafrija zote zimesitishwa ili kuungana na wafiwa kuomboleza msiba mkubwa uliyotokea katika taifa.

“Nawasihi wananchi wakati huu siyo wakati wa kutupiana lawama au kueneza habari zisizothibitishwa, sote tushirikiane pamoja na tukubali kuwa msiba huu ni amri ya Mwenyezi Mungu na umeandikwa kuwa mtihani kwetu,” alisema Dk. Shein.

Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote waliojitokeza kusadia kuokoa watu katika ajali hiyo na kuwataka wafiwa kuwa na moyo wa subira wakati wote wa maombolezo ya msiba huo.


Habari  NA MWINYI SADALLAH
Picha  - Chingaone Blog library
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Anonymous said... 21 July 2012 at 01:20

Dah hii ajali inasikitisha sana na Mungu azirehemu roho za marehemu mahala pema peponi Amina.

Michael Minja said... 21 July 2012 at 01:32

Naitwa MICHAEL MINJA kutoka ITALY: Nawapa pole ndugu jamaa na marafiki wote waliopoteza wapendwa wao katika ajali huu ya meli.

 
Top