Menu
 

•  Ni mwanasheria aliyesimamia ubomoaji wa mahekalu Kunduchi

na Betty Kangonga
KASI ya vitendo vya utekaji nyara inayotokana na visasi na chuki miongoni mwa jamii, inazidi kushamiri nchini, hususan jijini Dar es Salaam, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
 
Wakati wananchi wengi bado wana kumbukumbu ya tukio la kutekwa, kuteswa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, takriban wiki mbili zilizopita, tukio lingine la aina hiyo limemkumba Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Mazingira Nchini (NEMC), Manchere Heche.
 
Heche ni mmoja kati ya watendaji wa NEMC waliosimamia mpango mzima wa ubomoaji wa mahekalu ya baadhi ya vigogo waliojenga kandokando ya mito ya Mbezi Beach, Mndubwe na eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikoko ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam.
 
Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka chanzo cha karibu na mwanasheria huyo, zilidai kuwa mwanasheria huyo alitekwa nyara hivi karibuni katika eneo lilelile alilotekwa nyara Dk. Ulimboka la Leaders Club majira ya saa 4:00 usiku wakati walipoenda kupata vinywaji na chakula. Siku ya tukio, mwanasheria huyo aliongozana na wadogo zake.
 
Akiwa katika eneo hilo, ghafla liliibuka kundi la watu zaidi ya kumi na kumkamata mwanasheria huyo mithili ya kibaka na kumpeleka eneo la giza na kisha kuanza kumpiga.
 
“Yaani tulishangazwa na jinsi watu hao walivyokuwa mahiri kwa kuzingira gari na kusema kuwa sisi tunauza tiketi bandia jambo ambalo liliwastaajabisha wale waliokuwa karibu,” kilisema chanzo hicho.
 
Mtoa habari wetu alisema kuwa Heche alipelekwa eneo ambalo lilikuwa na giza totoro na kupigwa huku wakijaribu kumsukumia ndani ya roli lililopaki jirani na eneo la Uwanja wa Leaders Clab.
 
Hata hivyo chanzo hicho kilisema mwanasheria huyo alipambana vilivyo na watu hao kabla ya kuokolewa na mzee mmoja aliyekuwa akipita eneo hilo.
 
“Yaani hiyo ndiyo ilikuwa pona yake maana bila yule mzee sijui walitaka kumpeleka wapi hata hatuelewi…hata hivyo tunashanga kwa nini suala hilo linaibuka sasa maana lilitokea kitambo,” alisema mtoa habari wetu.
 
Habari zaidi juu ya tukio hilo zilisema kuwa watekaji hao walidhamiria kufanya uovu mkubwa kwani walikuwa wamebeba tindikali ambayo pengine ilikuwa itumike kummwagia mwanasheria huyo.
 
Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay ambapo mwanasheria huyo alipewa PF3 na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na majeraha aliyoyapata.
 
Inaelezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanasheria huyo alikuwa akipokea simu na ujumbe wa vitisho kupitia ujumbe mfupi wa mkononi tangu NEMC ilipoanza taratibu za kutaka kubomoa mahekalu ya vigogo wa eneo la Mbezi Beach.
 
“Siku moja wakati akitoka kazini akiwa njiani ghafla alikutana na watu waliokuwa katika gari walisimama na kumtahadharisha kuwa aache kuvunja nyumba alizokusudia na kama angeliendelea basi naye angelibomoka kama ambavyo angelibomoa nyumba hizo,” kilidai chanzo hicho.
 
Hata hivyo taarifa zilizozagaa jana majira ya asubuhi katika mitandao ya kijamii zilidai kuwa mwanasheria huyo alitendewa unyama huo mara baada ya kutekeleza msimamo wa kubomoa nyumba zilizojengwa katika mikoko.
 
Tanzania Daima Jumatano lilimtafuta mwanasheria huyo ambaye alikiri kukutwa na tukio hilo, lakini alisema lilitokea muda mrefu na vyombo vya ulinzi na usalama vilijulishwa.
 
‘Ni kweli tukio hilo lilitokea, lakini ni la muda mrefu. Hata hivyo sina la kuongea maana tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Terezya Huvisa, ameshalizungumzia.
 
“Kama unataka taarifa zaidi fanya mawasiliano na polisi maana wana taarifa zote lakini kiukweli niliumizwa sana na ni hatari iwapo wataalam tunafanyiwa unyama kama huu wakati wa kutekeleza majukumu yetu,” alisema.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa limeripotiwa katika ofisi yake na vijana wake wanaendelea na uchunguzi.
+
 
“Ni kweli hilo tukio lipo lakini ni la muda mrefu naomba unipe nafasi kesho (leo) nitakuwa na taarifa zaidi ya mahali lilipofikia maana bado tulikuwa tunaendelea na uchunguzi,” alisema Kamanda Kenyela.
Chanzo: Tanzania Daima

Post a Comment

 
Top