Menu
 


Kocha mpya Yanga, Tom Saintfiet (wa pili kulia), akiwa amezungukwa na baadhi ya mashabiki wa Yanga muda mfupi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga 

KOCHA mpya wa Yanga, Tom Saintfiet (39) ametua nchini jana mchana, akitanguliza kauli kwamba, atatumia uzoefu wake kimataifa katika taaluma ya ukocha kuleta mageuzi makubwa ndani klabu hiyo ya Jangwani.Saintfiet, raia wa Ubelgiji alitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kulakiwa na mamia ya mashabiki wa Yanga wakiongozwa na Katibu Mkuu, Celestine Mwesingwa.


Akizungumzia ujio wake, Saintfiet atakayerithi mikoba ya Kostadin Papic, alisema anaifahamu Yanga muda mrefu baada ya kuifuatilia katika mitandao pamoja na mashindano ya Kagame.

"Mimi siyo mgeni na Soka la Afrika, nalifahamu vizuri nimefanya kazi Nigeria, Zimbabwe, Namibia na Ethiopia. Kwa sababu hiyo, sioni kikwazo cha kushindwa kufikia malengo yangu.

"Isitoshe habari za Yanga na soka la Afrika Mashariki nazifahamu kupitia kusoma kwenye tovuti mbalimbali.

"Mwaka jana nilifuatilia kupitia kituo cha Super Sport  kilichokuwa kinarusha mashindano ya Kagame," alisema Saintfiet.

"Zaidi natarajia kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa uongozi na mashabiki ili kazi yangu iwe rahisi kuitekeleza."

Baada ya kuzungumza na wanahabari, Saintfiet alipanda katika gari aina ya Land Cruiser mpaka makao makuu ya klabu akisindikizwa na msafara wa mabasi madogo matatu.

Makao makuu, Mtaa wa Jangwani, Saintfiet alifanya mazungumzo mafupi na Mwesigwa kisha akaelekea kwenye ukumbi  na kuwasalimu mamia ya mashabiki waliokuwapo kumlaki.

"Nashukuru kwa mapokezi mazuri mliyonipa, kilichobaki ni kufanya kazi iliyonileta ili Yanga iweze kufikia mafanikio," alisema Saint Fiet.

Kwa mujibu wa msemaji wa Yanga Louis Sendeu, leo asubuhi Saintfiet atakutana na uongozi wa Yanga kwa mazungumzo kabla ya  kusaini mkataba.

Wakati huohuo, habari zilizolifikia Mwananchi jana jioni zilidai kuwa  Yanga imeondolewa  katika michuano ya Kombe la Urafiki inayoendelea mjini Zanzibar baada ya kukiuka masharti ya waandaaji.

"Tumeiondoa Yanga katika mashindano yetu ya Urafiki kutokana na kwenda kinyume na maelekezo ya barua ya mwaliko.

Tuliwataka kuleta timu itakayocheza michuano ya Kombe la Kagame, lakini wamefanya kinyume chake kwa kuleta  timu B.

"Wametusababishia hasara kubwa, mashabiki wamekasirishwa, hawana tena hamu ya kuja uwanjani," alisema msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria.

Walipoulizwa viongozi wa Yanga hawakuwa tayari kusema lolote kwa madai kuwa walikuwa na jukumu kubwa la mapokezi ya kocha wao mpya.

Katika hatua nyingie, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) jana ilitoa kiasi cha Sh20 milioni kwa ajili ya kufanikisha maandalizi ya  Uchaguzi Mdogo kuziba nafasi zilizoacha wazi kufuatia uongozi wa awali kujiuzulu.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam Julai 14 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.

Akikabidhi hundi jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe alisema pesa hizo ni sehemu ya udhamini wa TBL kwa Yanga.

Kuzaliwa:
29-3-1973
Timu za Taifa:
Namibia,
Ethipia,
Zimbabwe
Qatal
Klabu:
Al Gharafa (Qatal)
Rops(Finland),
B71 (Visiwa vya Island)
BV Cloppenburg ya Ujerumani.
Habari na - Sosthenes Nyoni na Clara Alphonce

Post a Comment

 
Top