Menu
 

BARAZA la Madaktari Tanganyika limewafutia usajili madaktari wote waliokuwa katika mafunzo ya vitendo  (Internship), baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mgomo wakiwa kazini.Taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa Dar es Salaam jana imeeleza kuwa madaktari 319 wamepoteza sifa ya kuendelea na taaluma hiyo hivyo usajili wao umesitishwa rasmi kuanzia jana.Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk Donan Mmbando amewataka madaktari hao kurudisha hati zao za usajili wa muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari.

“Kwa kuzingatia masharti ya sheria kuhusu kupata usajili wa muda, Baraza la Madaktari Tanganyika limeridhia kwamba madaktari wote ambao walijihusisha na mgomo, wamepoteza sifa na kwa sababu hiyo usajili wao umesitishwa kuanzia tarehe 11 Julai, 2012.”

“Madaktari wote wanaohusika wanatakiwa kurejesha hati za usajili wa muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari kabla ya terehe 17 Julai, 2012.”

Dk Mmbando alisema, awali Baraza hilo lilipokea malalamiko kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwamba baadhi ya madaktari waliopata usajili wa muda ili kuwawezesha kufanya mafunzo kwa vitendo (Internship), waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kati ya Juni 23 na Juni 29 mwaka huu.

Alisema madaktari hao walipangiwa kutoa huduma katika Hospitali za Muhimbili, KCMC, Rufaa Mbeya, Sekou Toure na Bugando za Mwanza, Amana, Temeke na Mwananyamala za Dar es Salaam, Haydom - Arusha, St Francis-Ifakara na Dodoma.

Alisema kutokana na mgomo huo, uongozi wa hospitali husika uliwaandikia barua iliyomtaka kila daktari aliyeshiriki kwenye mgomo huo kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.Dk Mmbando alisema kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa kwenye Baraza hilo, Msajili wa Baraza, alimwandikia kila daktari aliyelalamikiwa Taarifa ya Kusudio la kufanya Uchunguzi dhidi yake, juu ya malalamiko yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Alisema baada ya kuyafanyia kazi malalamiko hayo, Baraza limebaini kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madaktari, Sura ya 152, madaktari waliokuwa kwenye mgomo na ambao kwa sasa wameondolewa katika hospitali walizokuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo, wamepoteza sifa za kupata usajili wa muda.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk Edwin Chitage alisema alikuwa hajapata rasmi taarifa hizo licha ya kusikia fununu... “Sijapata taarifa rasmi lakini ni jambo tulilolitarajia na hatutashangaa tukisikia hilo kwa sasa subiri nithibitishe halafu nitatoa msimamo wetu.”
Kiongozi wa madaktari kortini

Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kudharau amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ya kuwataka kusitisha mgomo kupitia vyombo vya habari.

Amri hiyo ilitolewa Juni 22, mwaka huu na Jaji Sekela Moshi na kuwataka madaktari kurejea kazini mara moja, lakini amri hiyo haikutekelezwa.

Jana, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alimsomea Dk Mkopi hati ya mashtaka na kumweleza Hakimu Faisal Kahamba kuwa kati ya Juni 26 na 28, mwaka huu, Dk Mkopi akiwa Rais wa MAT, alidharau amri  iliyotolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi Juni 26, mwaka huu ikimtaka kutoa tangazo kwa wanachama wa chama hicho kupitia vyombo vya habari kwamba wasishiriki katika mgomo.

Kweka alidai kuwa Juni 27, mwaka huu Dk Mkopi aliwashawishi wanachama kushiriki kufanya mgomo kitu ambacho ni kinyume na amri iliyotolewa Juni 26, mwaka huu.

Hata hivyo, Dk Mkopi alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kiongozi huyo wa madaktari yupo nje kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 8, mwaka huu itakapotajwa na kuangaliwa kama upelelezi utakuwa umekamilika au la. 

Afya ya Dk Ulimboka
Wakati huo huo, afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka imezidi kuimarika. Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage alisema jana kwamba: “Tofauti na ilivyokuwa mwanzo, kwa sasa afya yake imezidi kuimarika, anakula mwenyewe lakini pia anazungumza mwenyewe na rafiki zake wa hapa nchini kwa  njia ya simu.”

Katika siku za karibuni, hali ya Dk Ulimboka ilielezwa kubadilika ghafla na kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kutokana matatizo mbalimbali, yaliyotokana na kupigwa ikiwamo figo kushindwa kufanya kazi.

Alisafirishwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi Juni 28, mwaka huu kwa ushauri uliotolewa na jopo la madaktari lililokuwa likimhudumia.

UN yanena
Katika hatua nyingine, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Dk Alberic Kacou amepokea barua ya MAT kuomba ulinzi kwa Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu Afrika Kusini kwa madai kuna kikosi kilichotumwa kuhakikisha harudi nchini akiwa hai.

Akizungumza jana Dar es Salaam jana, Dk Kacou alisema suala hilo la kutoa ulinzi watalitoa baada ya kuwasiliana na wote waliohusishwa kwenye waraka wa ombi hilo.

Mgomo wamalizika
Mgomo uliokuwa ukiendelea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (Moi), Dar es Salaam umemalizika na huduma katika hospitali hizo zimerejea kama kawaida jana.

Waandishi wa habari waliotembelea hospitali hizo waliona wagonjwa wakiwa wanaendelea kupokewa na kupatiwa huduma kama ilivyokuwa awali, kabla ya mgomo uliodumu kwa takriban majuma mawili yaliyopita


Habari na Tausi Mbowe, Tausi Ally, Leon Bahati na Issa Lazaro, Geofrey Nyang’oro

Post a Comment

 
Top