Menu
 

 Mh. Rais Kikwete akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji safi na upimaji wa maji katika Kijiji cha  Swaya,Wilaya ya Mbeya vijijini Julai 22 mwaka huu. 
********* 
Na Bosco Nyambege Mbeya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itamchukulia hatua kali za kisheria  mwananchi yeyote atakayebainika kuharibu  vyanzo vya maji nchini. 

Onyo hilo limetolewa hivi karibuni  na Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,alipokuwa akizindua mradi wa maji safi na upimaji wa maji katika Kijiji cha  Swaya,Wilaya ya Mbeya vijijini Julai 22 mwaka huu. 

Amesema uharibifu wa vyanzo vya  maji hupelekea kukosekana kwa maji na hivyo kusababisha majanga mbalimbali kwa binadamu kama vile ukame,magonjwa pamoja na vifo. 

Aidha amesema ili kuthibiti tatizo hilo la uharibifu wa miundombinu ya maji ni vema kila mtu akahusika kulinda vyanzo vya maji vinavyomzunguka, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika waharibifu wa vyanzo vya maji wanapobainika.

Amebainisha kuwa serikali itahakikisha inatatua tatizo la uhaba wa maji hapa nchini ili kumwezesha mwananchi wa kipato cha chini kupata maji safi na salama kwa wakati muafaka. 

Mbali la hilo Rais  Kikwete amewasihi wananchi kulipa bili za maji kwa wakati muafaka ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi na wakati.

Mradi huo wa maji umegharimu kiasi cha shilingi 79.5 bilioni mpaka ulipokamilika na unatarajia kuhudumia watu zaidi ya laki tatu mkoani mbeya  kwa muda wa miaka mitano ijayo. 

Mradi huo umejengwa kwa udhamini kutoka Ujerumani,umoja wa ulaya-EU kwa Ushirikiano na serikali ya Tanzania mpaka kukamilika kwake.

Post a Comment

 
Top