Menu
 

Na Esther Macha,Mbozi
Wakulima wa Kijiji cha Ichesa Kata ya Myovisi ,Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya wamelalamikia kuumwa matumbo baada ya kula ugali unaodaiwa kutokana na mbegu feki ya  mahindi ya njano inayodaiwa kusambazwa na wakala mmoja kijijini hapo.

Kutokana na adha hiyo wakulima hao wameziomba mamlaka husika na watafiti kulifuatilia kwa kina suala la ununuzi wa vocha za mbolea ya ruzuku kutoka kwa wakulima kumuuzia wakala kwa bei ya kati ya sh.2,000 hadi Sh.4,000 unaodaiwa kufanywa na wakala mmoja jina limehifadhiwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ichesa (majina tunayo)walisema kuna hatari kubwa kwa mwaka huu waananchi wa Kijiji hicho kukumbwa na baa LA njaa na hali ya uchumi kushuka kutokana na kusambaziwa mbegu inayotoa unga wa njano inayodaiwa ya kampuni ya pannar na hivyo kukosa kabisa soko.

Bw.Nasibu Mwashilindi alisema wamejitahidi kwenda kuuza mahindi hayo kwa sh. debe sh.2,000 katika soko la mazao Mlowo licha ya bei ya mahindi kwa debe kupanda hadi kufikia sh.6,000 lakini hayanunuliwi na kurudi nayo majumbani.

"Hali ni mbaya ndugu zangu haya mahindi ni shida kwani hakuna anayenunua kutokana na ugali wake kuwa mchungu mdomoni na hata upande wa soko bado ni tatizo sana sisi wananchi wa kijiji cha Ichesa tuna wakati mgumu sana kwani uchumu wetu wa maisha ni mgumu kufuatia hali hii kwani hatujui haya mahindi tutayapeleka wapi mpaka sasa"alisema mwananchi huyo.

Bw.Mwashilindi alisema kibaya zaidi mahindi hayo hayaliki kutokana na uchungu wa ugali wake hasa ukipoa na wengine wanalalamika watoto wao kuumwa matumbo wanapokula jambo ambalo wamehofia kuwa linaweza kuleta athari kiafya.

Baadhi ya wakulima walifafanua kuwa mbegu hizo zilizokuwa rangi ya njano wameuziwa na wakala huyo ambapo mfuko umeonesha zimetoka katika kampuni ya Pannar lakini katika jambo la kushangaza hata kibunzi ni chekundu na imefikia hatua wananyanyapaliwa katika mashine za kusaga kama watu wenye kimela cha kutengenezea pombe.

"Tunapokwenda kusaga mashine wanatuambia tusubiri hadi wamalize kusaga wenye mahindi meupe na sisi ndiyo tunakuwa wa mwisho hata kama tumewahi,sababu ni kwamba nikitangulia mimi mwenye mahindi ya njano na wote watakaofuatia hata wakiwa na mahindi meupe yanabadilika kuwa njano,"walisema.

Akizungumzia malalamiko hayo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ichesa,Bw.Paul Mwasenga alisema walipokea vocha za ruzuku za pembejeo 600 za mbolea aina ya Urea ya kukuzia mwezi februari,2012 na kwamba kweli vocha za mbolea ya kupandia aina ya CAN hazikufika kabisa.

Bw.Mwasenga alikanusha kusikia taarifa ya wakala kununua vocha za ruzuku kwa Sh.2,000 amekanusha vikali na kudai hizo ni njama za kuchafuana kisiasa na hakuna kitu kama hicho ingawa alifafanua.

Mtendaji huyo amekiri kupata malalamiko ya kuwepo mbegu feki ya mahindi ambayo imekuja kubainika baada ya mahindi kukomaa na kwamba wakulima walinunua mbegu hiyo katika maeneo tofauti ikiwemo kwa wakala Ntandala wa Kijiji cha Ichesa ambaye ndiye alikuwa akisambaza Kata ya Myovisi.

Katika suala hilo wananchi walisema Wakala huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji aliwashawishi wananchi kumuuzia vocha ambazo zote alikuwa ameshazisaini kwa bei hiyo hali iliyowafanya baadhi ya wakulima kumuuzia baada ya kuona hazina umuhimu tena kutokana na mbolea aina ya Urea kuchelewa kufika na Can kutokufika kabisa ilhali mazao yameshaanza kukomaa.

Mjumbe wa kamati ya ugawaji wa vocha ya Kijiji cha Ichesa,Bw.Mashaka Mwashambwa alisema hajawahi kusikia madai hayo na kazi wanayoifanya kamati ni kubwa kwani kabla ya kugawa wanatoa elimu kuhusu thamani ya vocha na punguzo lililotolewa na serikali baada ya kuitisha mkutano wa hadhara na baadaye walitembelea mashamba na kugawa vocha kwa wahusika.

Hata hivyo wajumbe wengine watano kati ya sita akiwemo Mwenyekiti na Katibu wa Kamati ya Vocha ya kijiji cha Ichesa hawakuweza kupatikana kuelezea sakata hilo.

Ofisa kilimo Kata ya Myovisi Bw.Danfod  Mandali   amethibitisha kupokea malalamiko ya mbegu feki  na hivyo alichukuwa hatua ya kuwasiliana na Ofisa wa kilimo Wilaya ya Mbozi ambaye alifika na timu ya wataalamu waliwahoji wakulima na kuchukua sample.

Bw.Mandali alisema  suala la madai ya baadhji ya wakulima kuuza vocha kwa wakala halijamfikia rasm,i ila kuna tetesi mitaani wakulima wakiwataja wenzao wanaolalamika kuuza kwa bei ya chini vocha hizo baada ya kuziona hazina kazi tena kutokana na mazao yao kukomaa.

"Wakulima ni kama asilimia 40 walioathirika na mbegu hiyo na kuhusu kuuza vocha  nimewahi kuwasikia wakulima wakiwataja wenzao waliouza kwa wakala huyo  lakini wanaficha ficha kuhofia kukosa kupata katika msimu unaokuja  kwa sababu kisheria ni makosa...huku ilikuja UREA tena kwa kuchelewa mwezi Machi,mbegu na mbolea ya kupandia walisema imehifadhiwa mkoani watapewa mwezi septemba, kwa ajili ya msimu wa 2012 na 2013,"alisema.

Wakala aliyedaiwa kugawa mbegu na kununua vocha katika kijiji cha Ichesa, Bw.Japhet Ntandala alipohojiwa kuhusiana na tuhuma hizo alikanusha na kulaani vikali kwamba wanataka kumchafua mbele ya wananchi wake na kwamba yupo tayari kununua mahindi yote kwa wale aliowauzia mbegu ili wananchi wake wasife na njaa.

Wakala huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kijiji hicho alisema hajawahi kununua vocha na angependa mtu aliyedai amemuuzia ajitokeze ili azungumze ukweli na yupo tayari kufika naye mahakamani ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.

Ofisa Kilimo Mkoa wa Mbeya ,Dkt.Philipo Mwaisoba alishukuru kupata taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia huku akidai ni hatari kubwa endapo vocha za ruzuku zimeuzwa tena kwa wakala kwani ni makosa kisheria na kwamba atafuatilia kujuwa mbegu hizo zinazodaiwa feki na kutolea majibu.

Jitihada za kuwasiliana na Kampuni ya Pannar na watafiti,Mamlaka ya chakula na dawa zinaendelea ili kubaini jitihada zinazofanywa ili kunusuru maisha ya watu wa Kijiji cha Ichesa na maeneo mengine ya wilaya ya Mbozi ambayo yanadaiwa kusambazwa mbegu hizo feki.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kuna taarifa ya kusambazwa kwa mbegu hizo feki karibu maeneo mengi ya Wilaya ya Mbozi na kuna hofu ya wananchi walio wengi kupata madhara ya kiafya na hali ngumu ya maisha kutokana na mahindi hayo kukataliwa na wanunuzi wa mazao.

Post a Comment

 
Top