Menu
 

Na Ester Macha.
Tunapozungumzia maji  kwa binadamu  ni pamoja na huduma hiyo kupatikana vijijini na mijini ambako mahitaji hayo ni muhimu kwa wananchi waishio maeneo  hayo lakini hali hiyo imekuwa tofauti kwa maeneo ya pembezoni na kujikuta wakiishi bila ya kupata huduma ya maji safi na salama.

Kutokana na hali hiyo  serikali ilitunga sera ya maji kwa kushirikiana na walengwa  kwa kubuni, kupanga, kujenga, kuendesha, kufanya matengenezo na kuchangia gharama za huduma utunzaji na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa kushirikisha wadau wote kwa kupunguza   majukumu ya utekelezaji kwa serikali ili kusimamia,kuratibu, kushauri, kuwezesha na kutoa miongozo.

Sera hiyo imekwenda tofauti kwa wananchi waishio vijijini na kusahaulika katika suala zima la maji safi na salama na kujikuta wakitumia maji machafu ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu ,lakini kutokana na shida ya maji hulazimika kutumia ili kuweza kukidhi mahitaji.

Muundo wa Sera  ya maji una sehemu kuu tatu za usimamizi wa rasilimali za maji kuweka na kuendeleza mfumo endelevu  na madhubutiwa kusimamia rasilimali maji Utoaji wa huduma ya majivijijini Kuboresha afya za wananchi wa vijijini, kuchangiakupunguza umasikini kwa kutoa huduma endelevu ya majisafi, salama na ya kutoshaUtoaji wa huduma ya majisafi na maji mijini Kuweka mfumo endelevu wa kutoa huduma kwa bei nafuu ili makundi yote yaweze kupata huduma ya maji.

Hivi karibuni timu ya wanahabari wanaharakati wa mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) walitembelea kijiji cha Ifiga kata ya Ijombe wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya  kujua tatizo la maji katika kijiji hicho jinsi linavyoathiri uchunmi wa wananchi wa eneo hilo .

Uhaba huo wa maji umekuwa sugu katika eneo hilo na kupelekea kutumia maji ya visima  ambayo si safi na salama na kujikuta wakiendelea kukumbwa na magonjwa ya kichocho  hasa kwa watoto na watu wazima.

Akizungumza na gazeti hili Mkazi wa Kijiji chsa Ifiga Bi.Sophia James anasema kuwa kisima hicho wamekuwa wakitumia wakazi 2000 wa kijiji hicho na kuwa pamoja na kuwa maji hayo si salama baadhi ya watu hasa watoto wamekuwa wakiyanywa pasipo kuchemcha  na hivyo kukubwa na maradhi ya tumbo.

Hata hivyo Bi.James anasema kuwa kutokana na hali hiyo ya tatizo la maji kijijini bado wamekuwa wakichangia wa  mradi wa maji bila mafanikio na hivyo kuomba serikali kusaidia kutatua tatizo hilo bila mafanikio .

Anasema wanawake wa eneo hilo  na watoto wamekuwa wakiathirika zaidi na tatizo la ukosefu wa maji kutokana na kisima hicho kuwa mbali na makazi yao hivyo wakati mwingine kutumia muda wa masaa manne hadi 6 kwenda kutafuta maji Kisimani .

Mwanamke huyo anasema kuwa  kutokana na tatizo hilo la maji wanawake walio wengi wameshindwa kuwa wazalishaji wazuri kutokana na muda mwingi kutumia kutafuta maji kwa kwenda uymali mrefu.

Aidha Bi.James anasema kuwa  kuachiwa majukumu zaidi ya kulea familia kwa kufanya kazi ya kusaka maji pamoja na shughuli nyingine za shamba huku baadhi ya wanaume wao wakishinda katika vijiwe wakisubiri kuhudumiwa na mwanamke.

Mwanamke mwingine Sevelena Mwahewa anasema tatizo la maji katuika kijiji cha ifiga ni kubwa  utokana wao kutembea umbali mrefu kutafuta maji ambako hata hivyo wakifika kunakuwa na foleni kubwa ambayo huwalazimu kusubiri kwa kupanga foleni.

“Tukiwa huko Kisimani inatubidi kukaa na kusubiliana kwa muda mrefu ambapo baada ya kuchelewa kurudi nyumbani waume zetu hutupiga na kuhoji tulikokuwa na kutoamini kama tulikuwa kisimani kusubiri maji,kwa ujumla hili ni tatizo kubwa kwetu  mimi mwenyewe ni moja wapo wa wanaume wa wanawake ambao nimepata kipigo kutokana na kuchelewa kurudui nyumbani”anasema Sevelena.

Hata hivyo anasema kuwa mara baada ya kupata vipigo hivyo kutoka kwa waume zao hushindwa kushtaki popote kutokana na kutishiwa na waume zao kuwa wasiseme popote . tatizo hili la maji limepelekea kuvunjika kwa ndoa nyingi kijini hapa.

Anaongeza  kuwa hata ukijaribu kumpeleka mahakamani mwanaume  jamii inayowazunguka humtenga mwanamke aliyemshtaki mumewe kuwa ni aibu kufanya hivyo.

Naye  Anna Mbalawala  Mkazi wa Ifiga anasema kuwa tatizo hilo la maji limeanza kujitokeza kati ya mwaka 2007 baada ya uongozi wa Halmashauri ya mji wa Mbeya kuanza mchakato wa kuwa jiji na hivyo kulazimika kuchukua mradi wa maji ambao ulichangiwa na wananchi wa kijiji hicho pia kwa kuchimba mtaro wa maji kutoka kijijini hapo na maji hayo kwenda kutumiwa na wakazi wa jiji la Mbeya.

Mwanamke Mwingine Bi.Frola Mlowezi anasema kuwa wananchi wa kijiji hicho kutumia maji ya kisima ambayo si salama watoto wake wawili wamekuwa wakitibiwa ugonjwa wa kichocho mara kwa mara kutokana na kutumia maji hayo ya kisima.

“Hii hali kwa kwali ni mbaya hapa kijijini kwetu tunaomba uongozi husika kutusaidia tatizo hili ili tuweze kupata maji ambayo ni salama vinginevyo hali hii inaweza kuwa mbaya kwa watoto wetu maji haya ya kisima ni machafu tunatumia basi tu hatuna jinsi”anasema.

Hata hivyo anasema aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya maji kijijini hapo Bw. Molis Selema anasema kuwa kabla ya mradi huo kuchukuliwa na jiji mwaka 2007 kulikuwa na kamati ya watumiaji maji ambayo kwa sasa ilivunjwa baada ya jiji kuchukua mradi huo.

Akizungumzia adha hiyo ya maji Mwenyekiti wa kijiji cha Ifiga Bw.Raphael Syejele anasema ni kweli tatizo hilo  maji lipo kijijini hapo alithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo la maji kijijini hapo na kuwa ugonjwa huo wa kichocho unachangiwa na huduma mbaya ya maji wanayotumia wananchi wake .

Anasema kijiji cha Ifiga kina wakazi 1175 wakiwemo watoto 748 na wazee 127 anasema kati ya wakazi wa kijiji hicho 636 ni wanawake ambao ndio wamekuwa wakitegemewa zaidi katika familia kwa kutumia kutafuta huduma hiyo ya maji.

Kuhusu kijiji cha Iwalanje wananchi wa kijiji hicho wamesema kuwa ni miaka 14 sasa hawajawahi kupata maji mpaka sasa licha ya kuendelea kuchangia maji,lakini hakuna mafanikio yeyote .

Bi. Marge John mkazi wa Iwalanje anasema kuwa wao wanailamu serikali kwani tuliambiwa tutachangie  asilimia 5 na tukakubali  lakini mpaka sasa hakuna dalili ya kupata maji mpaka leo.

“Tukiuliza kwa viongozi  wa vijiji  na kata  wanasema  wanafuatilia lakini kuna kipindi  Fulani walisema wakandarasi wamekosea kuchimba kisima cha maji hivyo bado tunasubiri”anasema.

Anasema kuwa maji wanayotumia wanachota Mto Shokwi  ambako hutoka saa 12 asubuhi na kurudi saa saba mchana  ambapo anasema hata hivyo katika Mto huo kuna Nyoka mkubwa aina ya Chatu ambaye ni hatari kwa maisha ya wanawake ambao ni tegemeo kwa familia.

 Aidha Mhandisi wa maji wilaya ya Mbeya Eng .Bahati Haule anasema kuwa bado serikali haina mpango wowote katika kijiji hicho kwa sasa katika kutatua kero ya maji wakati baadhi ya vijiji vya Iwalanje  vipo mbioni kutatua kero ya maji unafanyika.


Eng .Haule anasema kuwa hali ya upatikanaji wa maji safi kwa sasa katika Halmashauri ya Mbeya upo chini asilimia 50 na kusaema kuwa ipo mipango mbali mbali ya kutatua tatizo hilo baadhi ya maeneo huku akidai kuwa mbali ya kijiji cha Ifiga kutumia maji ya kisima bado kijiji cha Iwalanje pia wanatumia maji ya kisima.

Anasema kuwa Halmashauri imepokea fedha kutoka benki ya Dunia zaidi ya mil.800 kwa ajili ya kutatua kero ya maji katika kijiji cha Iwalanje na kusema kijiji cgha Ifiga wanasubiri wahisani waweze kusaidiwa .

Eng.Haule anasema kuwa maeneo ambayo yana matatizo ya maji katika wilaya ya Mbeya ni Mshewe ,Ipwizi,Chang’ombe,Mapogoro pamoja na Chelenje, Ifiga ambapo anasema utaratibu unaendelea ili maeneo hayo yaweze kupata maji.

Post a Comment

 
Top