Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Watu wanne wamefariki dunia katika Kijiji cha Mlangali,Chimali katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kufuatia gari walilokuwa wakisafirishia maiti kutoka Jijini Dar es salaam kuelekea Kyela mkoani hapa kupinduka majira ya saa 11 alfajiri.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja marehemu waliofariki katika ajali ya gari hiyo aina ya Toyota Land Cruiser kuwa ni pamoja na Essau Mwanitete,Lusako Mwakyanjala,Marwa Mokani na Constasia Essau.

Ameongeza kwa kuwataja majeruhi kuwa ni Bambombi Mwakyanjala,Atupele Izeck,Tukisigwe Mwakyanjala,Rose Meso,Anyandwile Philipo,Salemu Mwakyanjala na Amosi Mwanitete.

Aidha,Kamanda Diwani amesema Chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa na majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Chimala Mission na pia miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Katika tukio jingine la Ajali Mkazi mmoja wa Mji mdogo wa Tunduma,Wilaya ya Momba Mkoani hapa Elia Simon,amefariki dunia na wengine wawili kujeruhuwa vibaya baada ya kupinduka kwa gari walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe za Eid Elfitri.

Kamanda Diwani amesema marehemu alikuwa dereva wa gari hilo aina ya Toyota Hilux yenye nambari T. 816 AQH na kwamba ajali hiyo imetokea Agosti 20 mwaka huu,majira ya saa 12 kamilia asubuhi wakati wakitokea kwenye sherehe za Eid Elfitri,eneo la Maporomoko wilayani humo.

Hata hivyo ametoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani na wanapoendesha vyombo vya usafiri ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima na kwamba majeruhi wote wawili wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.

Post a Comment

 
Top