Menu
 

Habari na Hawa Mathias,Mbeya.
Mkazi wa Kijiji cha Mpona Wilayani Chunya  Mkoani Mbeya Joseph  Mwazembe(36) ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya ujambazi.

Tukio hilo limetokea Agost 21 mwaka huu majira ya saa 2 usiku katika Kijiji cha Mkatang’ombe,Kata ya Totowe wilayani humo ambapo ilielezwa marehemu alikuwa na wenzake wawili walivamia Grocery ya Hassan Michael (36) mfanyabiashara wa Kijiji cha Mpona.

Aidha mara baada ya kuvamia walipora simu za mkononi 15 ambazo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja na katika eneo la tukio kulikutwa risasi 5 za SMG na SR  na ganda moja  la risasi na panga alilokutwa nalo marehemu.

"Watu wawili ambao walidaiwa kuwa na marehemu walitoroka kwa kutumia pikipiki"alisema mmoja wa shuhuda ambaye hakutaka kutaja jina lake .

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa Diwani Athuman  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kutojichukulia sheria mikononi na kutoa ushirikino kwa jeshi la polisi kuwafichua waharifu wawili waliokimbia  na kuhusika katika tukio hilo.

Hata hivyo ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo jeshi la polisi limeweka mikakati ili kuhakikisha  mtandao huo wa uharifu unapatikana ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Post a Comment

 
Top