Menu
 

Mwandishi wa Makala hii:- Ester Macha,Mbeya.
MARA nyingi miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi imekuwa ikishindwa kufanikiwa kutokana na ukosefu wa fedha huku  ikiaminika kuwa Serikali haina fedha ya kutekeleza miradi hiyo.

Lakini hali hiyo imekuwa tofauti kwani baadhi ya wakuu wa idara katika halmashauri wamefannya sehemu ya fedha hizo kama saccos ya kukopeshana na kusahau kuwa fedha hizo zipo kusaidia miradi ya wananchi.

Pia hiyo haitoshi ndugu wa watumishi ambao walishafariki fedha hizo nazo zimekuwa kama sehemu ya saccos ndogo kwa wakuu hao wa idara lwakiamini kuwa hakuna anayejua hilo huku familia za ndugu hao zikiendelea kuneemeka na maisha magumu.

Ni dhahili kuwa kuna kila sababu kwa watumishi wa serikali kuanza kubadilika kwani kitendo hiki ambacho kinafanywa na baadhi yao ni cha aibu ambacho kinaitia aibu serikali na wananchi kukosa imani na watendaji hawa.

Mkoa wa Mbeya nao ni miongoni mwa halmashauri zake ambazo zimekubwa na kashfa hii lakini pengine yawezekana kuna mikoa mingine  zaidi ya mbeya ambayo inafanya hivi lakini bado kugundulika na pia  yawezekana huko ndiko kwenye ufujaji mkubwa sababu hakujafanyiwa uchunguzi wa kina ili kuweza kuwabaini waliohusika.

Nionavyo mimi binafsi ni kwamba Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali apite  kukagua halmashauri za mikoa mingine kukagua fedha za miradi ya maendeleo huenda huko ndiko kwenye uozo zaidi kwani watendaji wa serikali wamekuwa wakijimilikisha fedha za umma kwa kufanyia mambo yao binafsi na kusahau kuywa fedha hizo zipo kwa ajili ya kusaidia kuboresha miradi ya maendeleo huko vijijini.

Mi nadhani ifike wakati kwa watumishi wa serikali waanze kubadilika katika hili  kwani inaonyesha ni jinsi gani ambavyo watumishi wasivyokuwa  na nidhamu ya fedha za serikali kwa maana hiyo wamefika wakati mpaka kujikopesha fedha hizo pasipo kujali  lolote.

Licha ya ubadhilifu wa fedha za maendeleo bado baadhi ya watumishi wa halmashauri mbali mbali katika Mkoa wa Mbeya wamediliki kuchukua fedha za watumishi ambao walishakufa,kuhama,kufukuzwa kwa miaka mingi fedha hizo kuendelea kuingia katika akaunti za halmashauri na kuchukuliwa na wakuu wa idara ambao si waaminifu katika utendaji wao wa kazi.

Ifike wakati kwa  wakuu wa idara kuonyesha nidhamu hivi ni ujasiri gani ambao mtumishi anakuwa nao mpaka kufikia kuchukua fedha mpaka za wafu?ni ukweli usiopingika kuwa hii ni dalili mbaya kwa watumishi na pengine tabia hii ipo mpaka kwenye wizi fedha za walimu ila tu bado haijabainika .

Mfano katika Wilaya ya Mbarali kuna zaidi ya mishahara hewa zaidi sh.Mil.5,Mbeya Jiji zaidi sh.Mil.35.Wilaya ya Kyela mil.24 bado hizo wilaya zingine ambazo nazo bado zinapitiwa na mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali .

Nishauri kwa wakaguzi wafanye ukaguzi wa kina kwani inaweza kuna fedha nyingi ambazo zinachukuliwa kijanja na baadhi ya wakuu wa idara katika miradi mbali mbali ya maendeleo lakini hakuna anaye jua ,kama wameweza kuchukua mishahara mpaka ya wafu itashindikana vipi kuchukua fedha za miradi mingine?na nadhani kuwa endapo kungekuwa kunafanyika ukaguzi wa mara kwa mara ubadhilifu kama huu usingekuwa unakuwepo.

Lakini sasa kinachoniumiza zaidi bado wakuu hawa wa idara watabuni mbinu nyingine ya ubadhilifu wa fedha licha ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuwataka kurudisha fedha hizo ndani ya miezi miwili lakini bado naona
haitasaidia kitu kama ukaguzi huo umefanyika kwa mwaka 2011 mpaka 2010 hiyo miaka ya nyuma si fedha nyingi zimechukuliwa?.

Pia kitu kingine ambacho Bw. Kandoro amesema ili kuweza kudhibiti wizi huoni kuwa kila  halmashauri iandae  orodha ya watumishi wake ambao itapelekwa kwake  ikiwa na sahihi za watumishi wote wa halmashauri husika,hili sidhani kama inaweza kuwa dawa tosha kwa baadhi ya wakuu wa idara ijulikane kuwa hawa watumishi wanqa mbinu nyingi ya wizi wa fedha za umma.

Mi ninachoshauri ni kwamba utafutwe utaratibu mpya ambao utasaidia ubadhilifu huu ambao umekithiri kwenye mishahara hewa kwa watumishi kwa kuwaadhibu ambao watabainika kupitisha mishahara hewa hiyo kwa kiasi kikubwa itaweza kusaidia.

Nionavyo pia katika kutoa adhabu kwa baadhi ya wakuu hao wa idara  ni kwamba itafutwe adhabu ambayo itawafanya wawe na woga katika fedha za umma na si kwenye wizi wa mishahara hewa tu bali hata kwenye vyanzo vingine vya fedha za umma.

Lakini pia katika hili halmashauri ya Jiji la Mbeya kutokana na ubadhilifu huo wa mishahara hewa imeweza kufukuza watumishi wake sita na hii ni mara ya pili kwa uongozi wa jiji hilo kuwafukuza watumishi wake kwa ubadhilifu wa fedha katika hili napongeza uongozi mzima wa Mbeya jiji kuwa na ujasiri huu ambao halmashauri zimeshindwa kufanya hivyo licha ya mamilioni ya fedha kutafunwa.

Nadhani walichofanya halmashauri ya Jiji la mbeya kinatakiwa kuwa mfano tosha kwa halmashauri zingine kuona kuwa kuna umuhimu wa kuwachukulia hatua baadhi ya wakuu wa idara na kuachana na dhana ya kuwaonea aibu au kuwaogopa wahusika wakuu  waliofanya ubadhilifu.

Walichofanya Mbeya jiji  ni kizuri kwani  inaonyesha ni jinsi gani ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wakuu wa idara wanaobainika na makosa wanawafukuza kazi mara moja ili iwe fundisho
kwa watendaji  wengine.

Katika hili Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Bw. Juma Idd anatakiwa kuwa mfano na halmashauri zingine na kuachana na tabia ya woga iliyojengeka miongoni mwao kwa imani kuwa watarogwa  au kufanyiwa kitu chochote kibaya.

Endapo kutakuwepo na uwajibikaji kwa wakuu wa idara ambao wanabainika kufanya hivyo kwa kiasi Fulani itaweza kusaidia kupunguza ubadhilifu huo,kurudisha fedha zaa mishahara hewa haitoshi kinachotakiwa ni kupewa adhabu kali ambayo itakuwa fundisho kwa wengine.

Lakini pia nimekuwa nikijiuliza ni mara ngapi halmashauri zingine zimekuwa zikituhumiwa kubainika na wizi wa fedha za wananchi lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na watuhumiwa kuendelea kufanya kazi kama kawaida kwanini viongozi  wa halmashauri waliopewa dhamana wanashindwa kuwaadhibu watumishi hawa na badala yake kubaki
kuwakumbatia .

Hivi karibuni katika mikutano yake na watumishi wa halmashauri Mkoani hapa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro alisema hatakubali kuwajibishwa kwa halmashauri ambazo zitabainikqa kufuja fedha au
mishahara hewa .

“Nitahakikisha nakuwa bega kwa bega kwa zile halmashauri ambazo zitabainika kufuja fedha siwezui kukubali hata kidogo niwajibishwe mimi wakati waliotenda makosa wapo nitakufa nao”alisema.

Nionavyo katika kuhakikisha watendaji wanakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma hakuna budi serikali kupitia wakaguzi wake wa ndani kuhakikisha kuwa inafanya ukaguzi wa mara kwa ili kuweza kunusuru hali hii ambayo tayari imeota mizizi ndani yake.

Katika kila Mkoa na halmashauri imeweka wakaguzi wake wa ndani lakini cha kushangaza wakaguzi hao wapo ndani ubadhilifu ndo umekuwa mstari mbele sasa najiuliza  hawa watu wamewekwa kwa  ajili ya nini au ndo wapo kwa kushirikiana na wafujaji wa fedha hizo?

Sasa kama mtu upo na umewekwa kwa ajili ya kazi Fulani iweje uwepo katika kitengo hicho kuwa  kama pambo Fulani anafanya kazi wakati hata kuwajibika hakupo?mimi ninachokiona hapa ni kwamba hawa wakaguzi wapo kwa ajili ya kuwanufaisha baadhi ya wakuu wa idara ambao kazi yao ni kujichotea fedha za umma kwa manufaa yao binafsi.

Post a Comment

 
Top