Menu
 


Bw. Christopher Nyenyembe, ambaye ametetea kiti cha Uenyekiti katika uchaguzi huo
Ndugu zangu, nawasalimu katika misingi, miongozo na miiko ya taaluma ya habari, nikiamini kuwa kwa uwezo wa Mungu, mmlifanikisha kwa umahiri zoezi muhimu la kuiendeleza klabu ya wanahabari wa Mbeya (MBPC).

Kwa niaba yangu binafsi, Jukwaa Huru Media na wadau wengine wa habari ambao wanaitakia mema MBPC, napenda kuchukua wasaa huu kuwapongeza wale wote ambao wamefanikiwa kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali, nikiamini kuwa wanachama walioshiriki katika kufanikisha zoezi hili, walikuwa makini na walichagua kwa kuzingatia mahitaji ya klabu na mwanachama mmoja mmoja kwa upande mwingine. Pongezi kwa Bw. Christopher Nyenyembe, Bw. Mwazembe na Bi. Pendo Fundisha kwa kupita katika nafasi mlizokuwa mkiwania,pamoja na wajumbe wengine mtakaokuwa mkisaidiana nao.

Aidha, ni imani yangu kuwa, waliochaguliwa pia walikuwa wamejiandaa vyema kwa ajili ya sio tu kuchaguliwa, bali pia kuanza kuitumikia klabu haraka iwezekanavyo, punde tu watakapokuwa wamechaguliwa. Ni katika imani yangu hii ya pili ambapo nimeona nichukue fursa hii kuwapa matarajio yangu viongozi walioingia madarakani, nikiamini kuwa yatakuwa na mchango mkubwa katika kuzidi kuijenga na kuijengea heshima klabu hii.

Ndugu zangu,
Siku zote nimekuwa naamini kuwa, MBPC sio tu kuwa ni klabu ambayo imekuwa na mchango mkubwa sana katika kuleta mabadiliko kadhaa katika tasnia ya habari nchini na kwenye jamii kwa ujumla, bali pia, imejaaliwa kuwa na watu ambao wakijipanga sawasawa, wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi ya yanayowezakuonekana kwa sasa.

Yapo mambo kadhaa ambayo MBPC inaweza kujivunia kuwa ilikuwa mstari wa mbele katika kuyafanikisha ama kuanzishwa kwake, au kuyapa uzito na yakaonekana yenye tija, na ndio maana ninadhani umefikia wakati wa MBPC sasa kuwa kinara wa mabadiliko mengine makubwa lakini yatayokuwa na tija kwa upande wa wanachama wake na klabu kwa ujumla. Na hapa ni baadhi ya mambo ambayo ninaamini kuwa, umefikia wakati wa MBPC kuyafanyia kazi ili kuzidi kusonga mbele.

1. Mabadiliko ya Muundo wa Klabu:
Hili ni wazo ambalo limekuwa likinijia kila wakati. Nimekuwa nikijaribu kulizuia lakini limekuwa likizidi kunijia na ikafikia mahali nikawa nashindwa kulikwepa bali kulifikiria kwa marefu na mapana yake, na mwishowe nikaona ni wazo ambalo halina matatizo kwani litaiwezesha MBPC kusonga mbele.

Pamoja na mambo mengine, wazo hili limekuwa likihusisha kuifumua klabu toka mfumo wa sasa na kuingia katika mfumo wa shirikisho, kutokana na sababu kadhaa, lakini kubwa ikiwa ile ya muundo wa sasa kutokutoa fursa zilizo sawa linapokuja suala la baadhi ya vipaumbele vya MBPC na nitatolea mfano hili;

Pendo Fundisha, ambaye naye aliibuka kidedea katika uchaguzi huo – picha zote toka Maktaba
Kwa kadiri ambavyo dunia imekuwa ikisonga mbele, ndivyo ambavyo tasnia ya habari imeendelea kukumbwa na mabadiliko mengi, yakiwemo mabadiliko hasi na mabadiliko chanya. Wakati ambapo zamani tulizoea uandishi wa radioni na magazetini tu, siku hizi (kwa msaada wa teknolojia), kumeibuka machaguo mengi zaidi ya hayo yenye kujihusisha na habari kwa ujumla. Hapa namaanisha mitandao ya kijamii, mitandao ya mawasiliano, vifaa vya mawasiliano na mambo kama hayo.

Ni ukweli usiopingika kuwa, ujio wa Blogs/Weblogs/Websites, ni miongoni mwa mambo ambayo yameleta changamoto kubwa sana katika tasnia ya habari hususan kwa kuongeza wigo wa watu wenye kujihusisha na utoaji na usambazaji wa taarifa, ambao mwisho wa siku hawa wote, kimantiki, wanakuwa na sifa ya kuwa wanachama katika MBPC.

Haishangazi kuona kuwa, hivi sasa, miongoni mwa wanachama walio hai au ambao wangependa kujiunga na MBPC, wapo watangazaji, ma-DJs, Waandishi, Wapiga picha nk. Na ni mchanganyiko huu ambao unaleta swali la je, mfumo wa sasa wa MBPC na vilabu vingi, unaweza kuwa-accomodate wote hawa katika namna ambayo itakuwa na tija kwao na kwa umoja wao kwa ujumla?

Hebu, tuzungumzie suala la mafunzo, kwa mfano. Je, watu hawa wanahitaji mafunzo ya aina moja kila wakati? Kama ambavyo imezoeleka hivi sasa ambapo mafunzo huandaliwa kwa ujumla wake tu? Je, DJ, anahitaji mafunzo ya IJ katika kutimiza majukumu yake? Vivyo hivyo kwa makundi mengine ambayo nimeyaainisha hapo juu na yale ambayo labda nimeyasahau?

Katika mfululizo wa maswali, ndipo hapo najiuliza, je, hatuwezi kuweka namna ama mfumo ambao utaliwezesha kila kundi kunufaika kwa vipaumbele vyao (ambavyo mara nyingi, kama si zote hatujawahi kuvipa uzito), badala ya huu mfumo wa kufanya mambo kwa ujumla kama tulivyozoea hivi sasa?

Hatuwezi kuwa na mfumo ambapo DJs wataainishiwa vipaumbele vyao vya mafunzo na klabu ikashughulikia hilo kulingana na kundi husika? Hatuwezi kuwa na vipaumbele maalum kwa watangazaji, ambavyo vitafanyiwa kazi kiupekee kulingana na mahitaji yao? Vivyo hivyo kwa waandishi wa radio, TV, na wale wa mitandaoni ambao idadi yao inazidi kuongezeka siku hadi siku?

Ni katika mfululizo wa maswali ya namna hii, ambapo najiuliza Je, huu sio wakati muafaka sasa wa MBPC kuondoka katika mfumo wa klabu na badala yake ikawa katika mfumo wa shirikisho, ambapo makundi hayo niliyoyataja yanakuwa ndio wanachama wa shirikisho, litakalokuwa na kazi ya kuratibu tu mwenendo wa tasnia nzima kwa ujumla wake na sio ku-deal na mtu mmoja mmoja, ambao wanaweza kuwajibika katika vi-umoja vyao vitakavyoundwa kulingana na nafasi yao katika tasnia kwa ujumla wake?

Ndio, kwani hatuwezi kuwa na Umoja wa Watangazaji, Umoja wa DJs, Umoja wa Bloggers, ule wa Waandishi wa Magazeti nk? Na kisha viumoja hivi ndio vikawa vinawajibika kuratibu wanachama wake, huku Shirikisho (MBPC), likiwa na jukumu la kuandaa miongozo kwa makundi hayo badala ya mtu mmoja mmoja? Bilashaka, ninaamini kuwa, wazo hili tukiliboresha kwa kuchanganya mawazo yetu wote kama wadau, linaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko hasara.

2. MBPC Blog:
Nakumbuka kabla ya uchaguzi huu, niliwahi kuja na wazo la MBPC kuwa na Blog yake, ambayo ingekuwa na majukumu ya kuuhabarisha Umma mambo mbalimbali yenye kuhusiana na klabu kwa ujumla wake na wanachama wake mmoja mmoja kwa namna yao. Wazo hili, lilikumbana na kikwazo cha kuwa, lilikuja wakati wa kuelekea uchaguzi na ikahofiwa kuwa huenda ilikuwa sehemu ya kampeni. Na kwakuwa huo haukuwa mtazamo wangu, niliona ni heri niliache kwanza lisiendelee hadi uchaguzi upite.

Uchaguzi ule ulipita, na sasa tumefanya mwingine. Ni miaka sasaimepita, lakini hakuna hata mmoja wetu aliyekumbuka juu ya hili. Je, bado hatuoni umuhimu wa kuwa na Blog ya Klabu, hasa kwakuwa sote tunayajua manufaa na maslahi ya kitu hiki katika zama hizi? Ikumbukwe kuwa, Blog ya MBPC inaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato, kwani kama ikiendeshwa uzuri, ni wazi watajitokeza wadau kutangaza biashara na shughuli zao humo, na malipo yake kuwa sehemu ya mapato ya klabu.

Bibanfi, hili ni miongoni mwa mambo ambayo nahitaju kuona uongozi wa sasa ukiyafanyia kazi, kwani karibu kila kinachohitajika ili kufanikisha hili, kipo. Watu wa kuiandaa, watu wa kuiratibu na watu wa kufanya kila kinachohitajika ili kuiendeleza. Tuna bloggers kadhaa wenye kufanya uzuri sana katika upande huo hivi sasa, na ambao naamini wanaweza pia kufanya uzuri wakihusishwa kuendeleza project ya MBPC, mimi nikiwa mmoja wao.

Ndugu zangu
Yapo mengi ambayo ninatamani yafanyike, lakini kwa kuanzia naamini tukiyafanyia kazi haya mawili, MBPC itaendelea kuwa kinara wa mabadiliko kwa vilabu vya wanahabari nchini kwa ujumla wake. Ninaamini kuwa Uongozi ulioingia madarakani una uwezo wa kuyafanyia kazi haya, na nitakuwa tayari kutoa ufafanuzi au kukosolewa kwa pale ambapo mtazamo wangu utaonekana kuwa na mapungufu.

Nimeona ni heri niainishe kwanza matarajio yangu kwa uongozi mpya, badala ya kuupokea kwa kuanza kuchambua mapungufu ya uongozi huo, kama ambavyo imezoeleka sasa kuwa mara tu uchaguzi unapomalizika basi ndipo hapo hapo uchunguzi wa mapungufu ya watu unapoanza kujadiliwa, hali ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiifanya klabu kutokusonga mbele.

Ninawashukuru wale ambao watakuwa wameusoma ujumbe huu na kuuelewa huku nikiwapa pole pia kwa kuchukua muda wao mwingi kusoma hili. Ni imani yangu kuwa, uongozi na wanachama waliouchagua, tutashirikiana katika kusonga mbele na sio kuendekeza mambo ambayo si ya msingi
Hongera tena kwa waliochaguliwa kuingoza klabu. Na nawakaribisha kufanya kazi na Jukwaa Huru Media kupitia Jukwaa Huru Blog.

Wassalaam
Rama S. Msangi
CEO – Jukwaa Huru Media.
MAILTO: msangirs@jukwaahuru.com
WEB: www.jukwaahuru.com
 
Soma hapa pia kwa ujumbe zaidi>>>>> 

Post a Comment

 
Top