Menu
 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya Diwani Athumani,akizungumza suala la kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha walimu pamoja na walimu wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhamasisha wezao kugoma jambo ambalo ni kinyume cha sheria katika Mji mdogo wa Tunduma Mkoani Mbeya.
*******
Habari na Ezekiel Kamanga, Tunduma.
Watu 9 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya,wakiwemo viongozi wa Chama cha walimu na walimu wenyewe kufuatia vurugu zilizosababisha hasara zaidi ya shilingi milioni 100 wakati wa mgomo wa walimu ulioanza juzi.

Kitendo cha walimu hao kugoma kuingia madarasani kufundisha kwa kushirikiana na wanafunzi walifanya maandamano ya amani ya kudai haki ya masilahi ikiwemo mishahara na tukio linadaiwa kutumiwa vibaya na wahalifu kwani walitumia nafasi hiyo kufanya uhalifu kwa kuiba mali za watu.

Wahalifu hao walichoma ofisi za Halmashauri ya Mbozi ndani ya Mji mdogo wa Tunduma  na kuiba mali zilizokuwemo kama  kompyuta 5 za ofisi, pikipiki yenye namba STK 6264, kumbukumbu na nyaraka mbalimbali.

Wahalifu hao  walivunja milango ya ofisi zote, kuvunja vioo vya magari ya kubebea taka aina FAW  SM 8726, na kuiba betri mbili za gari hilo  na gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858 mali ya mamlaka hiyo.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani , aliwataja watuhumiwa hao wanaodaiwa kuhusika na uhalifu  na kusababisha hasara ya shilingi  milioni 117, 515,000  kuwa ni Mexon Mbilinyi(27) mkazi wa Mtaa wa Maporomoko, Akida Kondo(25) mkazi wa Mtaa wa Chapwa, Chalres Rupia(29) mkazi wa Mwaka,Athumani Mgala(39) mkazi wa migombani.

 Wengine ni Stela Garbert(20) mkazi wa Mtaa wa Migombani,Atiliyo Benard(28) mkazi wa Mkurungu nchini Zambia, Nikodemus Exavely(17), Mashaka Amoni(17) wote ni wakazi wa Mtaa wa Kaloleni - Tunduma na James Kabuje(29) mkazi wa Mtaa wa Mabatini - Tunduma.

Diwani, alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuhusika na uhalibifu wa ofisi ya halmashauri ya mji mdogo wa tunduma ikiwa na kuiba mali yenye thamani zaidi ya milioni 100 na kwamba wote kwa pamoja wamefikishwa mahakamani leo.

Akizungumzia suala la kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha walimu pamoja na walimu  alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na tuhuma za kuhamasisha wezao kugoma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Aliwataja wahusika hao kuwa ni Mwalimu wa Patro Mangula na ni Katibu wa chama cha walimu wilaya ya Kyela ambapo inadaiwa kuwa kiongozi huyo alikuwa akishirikiana na watu wengine kupita mashuleni kuhamasisha walimu waliokuwa wanaendelea na kazi ya kufundisha wajiunge na mgomo.

Wengine ni Mwalimu Emanuel Kyejo wa shule ya msingi Mbebe Wilaya ya Ileje na mjumbe wa chama cha walimu wilaya ya Ileje, Anyakingwe Lwinga na mjumbe wa chama cha walimu ambapo wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuhamasisha walimu kugoma.

Aidha, katika uhalifu wa Tunduma, Kamanada Diwani alisema kuwa polisi Mkoani Mbeya kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuokoa Mabati 168, Printa moja na mita mbili za maji, Bendera moja ya Taifa na photocopy mashine.

Pia, Kamanda Diwani alitumia nafasi hiyo kutoa ufafanuzi kwa nini askari wake walitumia  Bomu  na risasi katika vurugu hizo ambapo alisema kuwa Bomu hilo lilitumiwa kulitawanyisha kundi kubwa la watu lililokuwa linazidi kuelekea kwenye ofisi za serikali pamoja na Taasisi za kibenki  na kwamba hakuna madhara yaliyojitokeza.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakiipotosha jamii kuwa askari walitumia bomu kuwatawanya wanafunzi na ndio sababu za wananchi kuanzisha vurugu jambo hilo si kweli kwani bomu lilitumiwa baada ya kundi la wahuni lililokuwa likivamia ofisi na kuiba mali zilizomo ndani,”alisema.

Alisema,  wakati kundi hilo linafanya vurugu tayari wanafunzi walikuwa wamerejea kwenye makao yao lakini kundi hilo la wahuni ndio lilikuwa likizidi kujikusanya na kuendelea kufanya uhalifu huo huku baadhi wakiwa wanaelekea kwenye eneo la Benki.

“Baada ya walinzi wa Benki kuona kundi hilo linaikaribia benki askari walipiga risasi mbili juu ili kuwatawanya na kwamba zoezi hilo lilisaidia kuwarudisha watu hao waliokuwa na lengo la kufanya uhalifu katika benki hiyo ,”alisema

Aidha,  Diwani aliitaka jamii kuondoa mawazo potofu kwamba huenda vurugu hizo zimechangiwa na baadhi ya wanasiasa jambo ambalo si kweli kwani jeshi la polisi linaamini kuwa kundi hilo la uhalifu halina itikadi yoyote ya siasa.

“Polisi inawashikilia watu hao kwa tuhuma za uhalifu na ninaamini watu hawa ni wahalifu hivyo watafikishwa mahakani kwa makosa ya uhalifu tu na wala hakuna siasa,”alisema

 Hata hivyo aliwataka walimu pamoja na viongozi wa chama cha walimu kuacha kuwahamasisha wezao kufanya mgomo kwani wao tayari walitangaza kugoma na wamegoma hivyo kupita mashuleni na kuwakuta wezao wanafundisha na kuwalazimisha kugoma ni uvunjifu wa amani hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa zidi yao.

Kwa upande wao wanafunzi wakiiongea katika mkutano wa hadhara na wamewaomba walimu kurejea kazini kwani wanaathirika kimasomo kufuatia mgomo wao hali wakiwa wanajiandaa kufanya mitihani kwa darasa la nne,saba,kidato cha pili na nne.

Naye,Diwani wa Kata ya Tunduma kupitia tiketi ya CHADEMA  mheshimwa Frank Mwakajoka,amesema hujuma zilizofanywa na vibaka hao hali hiyo haitavumiliwa na kuwataka wakazi wa mji huo kuwa walinzi wa mali za umma,kwa kitendo hicho kimefanywa na watu ambao si wakazi wa Tunduma,hali inayopelekea wakazi kuathirika.

Ameongeza kwa kusema wale wote waliohusika na uhalifu huo kurudisha vifaa vilivyoibwa ili huduma ziendelee kama kawaida,ambapo baadhi ya bidhaa zimeanza kurudishwa  na kukabidhiwa Jeshi la Polisi.

Post a Comment

 
Top