Menu
 

 Sehemu ya Mwili wa Bwana Ibarahim Hassan Matipa, mkazi wa Kijiji cha Kongoro Mswiswi,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya ukiwa umejeruhiwa baada ya kupigwa kwa waya wa umeme na Askari wa Jeshi la Polisi PC Wiston, kwa kosa la kudaiwa kuiba pesa shilingi Milioni 4 mali ya Bwana  Lenard Mwampyate.
 Bwana Ibrahim Hassan anayedaiwa kushirikiana na wenzake sita kuiba pesa shilingi milioni 4,na kupigwa kwa kutumia waya wa umeme.
*****
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbarali.
Jeshi la polisi wilayani Mbarali mkoani Mbeya limeingia katika kashfa ya kutesa na kuzulu miili ya maabusu wanaokamatwa wakiwa salama na kufikishwa katika vituo vyao.

Hali hiyo imebainika baada ya mwananchi Ibrahim Hassan Matipa na wenzake kukamatwa Julai 30, 2012 kwa tuhuma za wizi wa Shilingi Milioni Nne mali ya Leonard Mwampyate alizodai kuwa alizihifadhi katika kiti cha gari yake aina ya Noah yenye nambari T 554 BQB ambayo ilikuwa imekodishwa kwenye harusi ikiendeshwa na mjomba wake Goliath Mwangonji kwa ajili ya harusi.

Akizungumza na mwandishi wetu Bwana Matipa alisema kuwa baada ya kukamatwa walipelekwa katika kituo cha Polisi cha Mswisi wilayani humo na kuanza kuteswa huku wakipigwa na waya za umeme katika miili yao.

Alisema kuwa wakati wanapigwa na askari waliyemtambua kwa jina la PC Wiston, walikuwa wakilazimishwa wakubali kuwa walihusika na tukio hilo la wizi na wao baada ya kuendelea kukataa ndipo wakaendelea kusulubiwa na askari huyo.

Aliwataja wenzake sita ambao nao walipata kipigo kutoka kwa askari huyo kuwa ni Ismail Omary na Rashid Mussa,wengine ni Bagaza Abubakari,Bwana Harusi Omary Mbago,Rashid Musa,Ally Mwangonji ambaye ni dereva na Saidi Silapola.
 
Kwa mujibu wa Askari huyo PC Wiston,amesema pesa hizo zimelipwa shilingi milioni 3 kati ya milioni 4 zinazodaiwa kuibwa na ndipo watuhumiwa wakaachiwa huru bila kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Haki za Binadamu mkoani hapa Bwana Said Madudu,amelaani vikali kitendo kilichofanywa na askari huyo na kwamba taarifa za tukio hilo zimeshafikishwa kwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Diwan Athuman alimuagiza Mkuu wa Upelelezi wa mkoa(RCO) kulishughulikia suala hilo kutokana na yeye kuwa nje kiofisi.

Post a Comment

 
Top