Menu
 

Na Nickson Mahundi,Njombe.
Sekta ya utalii katika Mkoa wa Njombe imeelezwa kusahaulika katika mkoa,licha kuliingizia taifa kipato kutokana na wageni mbalimbali wanaotembelea vivutio hivyo kwa ajili ya kujionea maajabu mbalimbali.

Licha ya mkoa huo kuwa na vivutio vingi vya utalii, ikiwamo hifadhi ya wanyama ya Kitulo, shamba la maua yenye kuvutia na kustaajabisha lilopo Uwemba  na mwamba wenye ramani ya afrika unaopatikana katika Kijiji cha Igodiva Tarafa ya Imalinyi Wilaya ya Wanging’ombe lakini hakuna kinachoendela.

Hata hivyo kutokuwapo kwa juhudi za kutosha katika kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio hivyo kumechangia vivutio vingi vya utalii kutofahamika hata kwa baadhi ya wenyeji wa mkoa huo, kwani wakazi wengi bado wanaamini kwamba sekta ya utalii hapa nchini ipo katika mikoa ya kusini pekee.

Akizungumza na gazeti hili afisa utalii, mali asili na mali kale wa wilaya ya Njombe Bw.Abed  Chaula alikiri kuwa  wakazi wa mkoa huu kutokuwa na mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo  hapa hali ambayo inachangia kutofahamika kwa vivutio hivyo kwa baadhi ya wakazi mkoa wa Njombe.

“Baadhi ya wakazi wengi wa mkoa huu hawana mwamko wa kutembelea vivutio vya utalii kwa kuzani kuwa anayepaswa kutembelea vivutio hivyo ni watalii kutoka nje ya nchi pekee, lakini wengine wako hapa mkoani hawajui vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa wakiamini kuwa fursa ya utalii ipo katika mikoa ya kusini pekee,” alisema Chaula.

Sanajari na hayo alikiri kutofanya jitihada za makusudi katika kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo mkoani hapa pamoja na kutoa hamasa ya kutosha kwa wananchi hususani wenyeji wa mkoa huo kutembelea vivutio hivyo vya utalii.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi wa Njombe kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii ili kuwa mabolozi wazuri wa vivutio hivyo.

“Nawaomba wakazi wa Njombe kuwa na utaratibu wa kutembelea vituo vya utalii, unajua ni aibu mgeni anakuja anakuuliza kivutio cha utalii kilichpo katika eneo lako halafu mwenyeji hukijui,’’ alisema Bw.Chaula.

Aidha Chaula alisema kukua kwa sekta ya utalii katika mkoa kutasaidia kupatikana kwa fursa nyingi za ajira na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

Baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa ni pamoja na mapango na misitu ya nyumba nitu, mwamba wenye ramani ya afrika wenye ukubwa wa hekari  saba, mpanga kipengele, hifadhi ya Kituro na Mdandu ambako kunapatikana boma la wajerumani na mahakama ya mwanzo iliyojengwa na wajerumani pamoja na mti mkubwa wa asili wa Mlizombe

Vingine ni safu ya milima ya Livingstone,misitu ya miyombo na fukwe za ziwa Nyasa vyote hivyo vinapatikana katika wilaya ya Ludewa katika mkoa huu wa Njombe.

Post a Comment

 
Top