Menu
 

Habari na Ester Macha,Mbeya.
Kufuatia mauaji  ya mwandishi wa habari wa  kituo cha Channel Ten  Mkoani Iringa Bw. Daudi Mwangosi Umoja wa klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umeitaka serikali kuwasimamisha kazi askari waliohusika katika tukio la mauaji ya kutisha ya mwandishi huyo.

Umoja huo umesema kuwa askari walioshiriki katika oparesheni  hiyo ambayo ni haramu wamesema serikali iwasimamishe kazi mara moja ili kupisha uchunguzi kufanyika.

Hayo yalisemwa jana  Jijini Dar Es Salaam na  Rais wa Umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania Bw.Keneth Simbaya wakati alipokuwa akitoa tamko  la mauaji  dhidi ya mwandishi wa habari aliyeuwawa akiwa mikononi mwa polisi katika kijiji cha Nyololo Wilayani Mufindi.

“Hapa tunataka uchunguzi  huu ukikamilika tunaitaka serikali  kuutangazia umma na kupisha sheria kwa wale watakaobainika  kuhusika kwa uzembe huo kwa namna moja au nyingine wachukuliwe hatua dhidi ya mauaji haya ya mwandishi wa habari Bw. Daudi Mwangosi”alisema.

Hata hivyo Bw. Simbaya alisema wakati uchunguzi ukiwa unaendelea  serikali iridhie  na kurasimisha  malipo  kwa ajili ya Mjane wa mwandishi huyo  na watoto walioachwa na marehemu ili waweze kujikimu.

Aidha alisema licha ya kutoa tamko hilo wanaendelea  kulitazamia jeshi la polisi  kama mdau  mwenye shaka namna wanavyotenda kazi  na waandishi wa habari  mikoani  na kwamba watataarifu umma kuhusu mwenendo wao hapo baadae.

“Lakini pia katika mkutano huu tumeridhia  kushirikiana na taasisi  zingine za haki za binadamu  ,uwakili na Utetezi ili kubaini  namna bora ya kuistaki serikali kama mwenendo wa suala hili  hautakuwa  unaleta tija hivyo tunakarisha mashirika  ya haki za binadamu ,asasi zisizokuwa za kiserikali ili kuweza kufanikisha azma hii”alisema Bw. Simbaya.

Akizungumzia kuhusu usalama kwa waandishi wa habari Bw. Simbaya alisema katika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa usalama amelitaka jeshi la polisi  kutoa utaratibu ambao  utawezesha wanahabari  nchini  kufanya kazi kwa usalama bila hofu wala dharau,kutoa elimu kwa jeshi la polisi  kuhusu  umuhimu wa wanahabari  na jukumu lao katika Taifa.

Hata  hivyo baadhi ya viongozi wa Vyama vya waandishi wa habari Tanzania  ambao wanahudhulio mkutano mkuu wa umoja wa clabu za waandishi wa habari Tanzania walisema tamko hilo halijapewa uzito kutokana na tukio la mauaji lenyewe jinsi lilivyo inatakiwa kupewa uzito wa kina.

“Hili Tamko lilitakiwa kupewa uzito sana kwani  sisi tuliokuwepo katika msiba huo kwa ujumla inasikitisha sana hivyo tamko ni muhimu lipewe uzito zaidi kulingana na mauaji yenyewe yanavyotisha  hivyo tufuate maamuzi ya viongozi wa clabu waliotoa matamko ya kususia habari za polisi mpaka pale watakapokuwa wameridhia  kukaa meza moja na wanahabari  juu ya mauaji hayo”alisema mmoja wa viongozi wa clabu za waandishi wa habari Tanzania Bw. Christopher Nyenyembe.

Post a Comment

 
Top