Menu
 

Na Angelica Sullusi,Mbeya
Wajasiliamali nchini wameiomba serikali kupandisha kodi kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nchi za nje  hususani zile zinazofanana na bidhaa zinazotengenezwa na wajasiliamali hao ili kulinda soko la bidhaa hizo nchini.

Ujumbe wa wajasilimali hao umetolewa jana katika risala yao iliyosomwa mbele ya Waziri wa Viwanda na Biashara ABDALAH KIGODA Jijini Mbeya jana katika Ufunguzi wa maonyesho ya wajasiliamali Nyanda za Juu Kusini yaliyoandaliwa na Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo(SIDO).

Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wenzake Rhoida Mwazembe aliiomba serikali kuhamasisha watanzania kupenda kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari hususani kuanzisha vipindi vya kuelimisha jamii kupitia radio na luninga.

Akijibu risala hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara Abdalah Kigoda alisema kuwa serikali inashughulikia tatizo la upatikaji mgumu wa mitaji kwa wajasiliamali hao hususani kupata mikopo yenye riba kubwa.

Aidha, Waziri Kigoda alitoa agizo kwa Halmashauri zote za Wilaya nchini kuhakikisha zinatenga haraka maeneo maalumu kwa ajili ya wajasilamali wadogo wadogo katika kuhakikisha wanapata eneo maalumu la kuuzia bidhaa zao.

“Natoa agizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalum kwa wajasiliamali hawa ili kukabiliana na changamoto wanayoisema ya kukosa mahali pa kufanyia kazi”alisema Kigoda.

Aliongeza kuwa serikali inatambua umuhimu wa sekta hiyo kwa kuwa inakuwa kwa kasi hivyo itajitahidi kuondokana na nadharia na kufanya mambo kwa vitendo zaidi.

Post a Comment

 
Top