Menu
 

*Ni katika shamba la Kapunga Rice Project.
*Wazazi wacharuka na kuanza kujenga shule mpya mahali alipobomoa mwekezaji.
*Zaidi ya shilingi milioni 2.5 zachangwa papo hapo.

Habari na Ezekiel Kamanga,Mbeya.
Wanafunzi 23 wa Shule ya Msingi Kapunga,Kijiji cha Mapogolo,Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya wamenusurika kifo baada ya kula mikate inayosadikiwa kuwa na sumu mnamo mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Ramadhani Nyoni na mzazi mmoja wapo wa watoto waliokumbwa na janga hilo la kusikitisha na kuhatarisha uhai.

Mzazi huyo ambaye hakupenda jina lake kutaja amesema yeye ilimlazimu kununua lita 20 za maziwa,kisha kuwanywesha watoto hao na kuokoa maisha yao ambapo hali zao zimetajwa kuendelea vema.

 Wakazi wa kijiji hicho wakionekana kukerwa na kitendo hicho iliwalazimu kuitisha mkutano wa hadhara na kuazimia kujenga shule mpya ili kuwaondoa watoto katika shule iliyopo katika shamba la mwekezaji.

 Mbali ya wananchi kukerwa na vitendo vya kikatili vya mwekezaji huyo,pia Walimu wamefurahia uamuzi wa wanakijiji kuamua kujenga shule mpya katika himaya ya kijiji ili kuondoa adha ya kutembea umbali wa kilometa 52 kwenda na kurudi kutoka Chimala,ambako ndipo walipopanga kutokana na uhaba wa nyumba kijijini hapo na zilizopo shambani kwa mwekezaji walimu hao hufukuzwa mara kwa mara.

Aidha wazazi hao waliachanga jumla ya shilingi 2,500,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi,ambapo Afisa Elimu kitengo cha Ujenzi amesema atawakabidhi ramani ya shule,uongozi wa kijiji,ili kuondoa adha ya wakazi zaidi ya 12,000 wanaoishi eneo hilo ambapo shughuli za maendeleo zimedumazwa na mwekezaji huyo ikiwemo kuhodhi miundombinu kama barabara,umeme na maji.

Licha ya miundo mbinu yote kupita kijijini hapo lakini wananchi hawanufaiki nayo bali kuambulia kipigo na kufunguliwa kesi mahakamani pasipo sababu maalumu.

Hata hivyo wananchi hao wamesema hawakuona sababu yoyote ya msingi kuweza kutoa taarifa katika Jeshi la polisi,kutokana na mwekezaji kujaza mafuta magari pindi magari ya jeshi hilo yanapoenda kijijini hapo.

Wananchi hao walienda mbali zaidi kwa kusema kuwa baadhi ya mifugo ya wananchi imekuwa ikiuawa mara kwa mara na mwekezaji huyo,lakini hakuna hatua zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa likiwemo tukio la wananchi kugongwa na gari la mwekezaji ambapo alimfukuza na kisha kumgonga mwananchi huyo,ambaye kwa sasa amepata ulemavu na mwekezaji kutochukuliwa hatua zozote tangu mwezi Julai mwaka jana.

Pia mwekezaji huyo mapema mwezi Januari mwaka huu alichoma mpunga wa wakulima kwa kunyunyizia dawa kupitia ndege ya umwagiliaji na kusababisha zaidi ya wananchi 150 kuathiriwa na sumu hiyo ya mimea na kuwasababishia hasara kubwa,ambapo njaa inatazamiwa kuwakabili wananchi hao.

Post a Comment

 
Top