Menu
 

Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
*Ni baada ya kukamatwa na Uongozi wa Kijiji.
*Chanzo ni Mishikaki ya Shilingi 1,000/=
Mkazi wa Kitongoji cha Gezaulole, Kijiji cha Haporoto Kata ya Ihango Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya Mbwiga Mwandele(50 -55)  amejinyonga kwa kutumia mkanda wa Suruali yake katika Ofisi ya kijiji hicho.

Tukio hilo limetokea Oktoba 26 mwaka huu majira ya saa mbili usiku na maiti yake kugunduliwa Oktoba 27 saa mbili asubuhi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa marehemu kabla hajafikwa na mauti alidaiwa deni la shilingi 1000 ambayo inadaiwa kuwa alikula mishikaki(nyama) eneo la Kilabu cha Kijiji cha Haporoto, ambapo huuza pombe za kienyeji na marehemu kushindwa kulipia mishikaki na kupelekwa katika Ofisi ya kijiji.

Aidha Uongozi wa Kijiji hicho chini ya Mwenyekiti wake Bwana Daimon Mndewa alimwachia jukumu mgambo wa kijiji hicho Bwana Fredy Wiston, kumlinda marehemu ili asubuhi ya Oktoba 27 suala hilo lizungumzwe lakini ilipofika asubuhi mgambo huyo alikuta Mwiga amejinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali aliokuwa ameuvaa marehemu kabla ya kifo chake.

Kwa upande wake  Mke wa marehemu Bi Malita Mbwiga(45) amesema waliachana na mumewe muda mfupi walipokuwa wakinywa pombe na yeye kuamua kurejea nyumbani na marehemu hakurejea nyumbani na baadae alipata taarifa ya kuwa kajinyonga katika Ofisi ya kijiji Oktoba 27 mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gezaulole Bwna Raphael Jailos Mbenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na mwili wa marehemu ulichukuliwa na jeshi la polisi hadi hospitali ya Rufaa jijini Mbeya na kwamba Jeshi la polisi linawashikilia Mwenyekiti wa kijiji na mgambo kwa mahojiano na kwamba wakati wa tukio Afisa Mtendaji wa kijiji Bwana Mwalingo Mbenya hakuwepo kijijini hapo.


Post a Comment

 
Top