Menu
 

NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.

EPHRAIM Mwaitenda amechaguliwa kwa kishindo, kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Mbeya mjini baada ya kuwabwaga vibaya wapinzani wake wawili waliokuwa wanawania nafasi hiyo.

Mwaitenda aliibuka kidedea kwa kupata kura 552, huku Emili Mwaluka akishika nafasi ya pili kwa kura 142 wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na Japhet Mwasanga aliyeambulia kura 108.

Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya mjini, Raymond Mwangwala, akizungumza na gazeti hili alisema uchaguzi huo uliofanyika uwanja wa Sokoine mjini hapa, ulihudhuriwa na wajumbe 1,016 na ulikuwa na utulivu mkubwa.

Mwangwala alisema katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), wilayani ilichukuliwa na kada maarufu Sambwee Shitambala, aliyepata kura 653 na hivyo kufanikiwa kuwabwaga kwa mbali Kamanda wa UVCCM mkoa, Dk.Stephen Mwakajumilo aliyepata kura 278, Fatuma Kasenga aliyepata kura 67 na Daniel Fussi aliyeambulia kura 17.

Kwa nafasi ya wajumbe wawili wa mkutano mkuu wa CCM mkoa, waliochaguliwa ni mwandishi wa habari wa kituo cha redio cha Generation Fm, kilichopo mjini Mbeya, Jackson Numbi na Tonebu Chaula.

Katibu huyo wa CCM wilaya ya Mbeya mjini, aliongeza mwandishi wa habari wa kampuni ya Business Times, mkoa wa Mbeya Charles Mwakipesile, aliibuka kidedea kwa kupata kura 630 katika nafasi ya wajumbe kumi wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya.

Wengine walioshinda katika nafasi hiyo ni Fatuma Kasenga, Edina Mwaigomole, Odran Chaula, Benjamin Balali, Henje Mwalungwe, Maria Nyagawa, Isaack Sintufye, Godfrey Habaya na mmliki wa kituo cha redio cha Generation Fm, Shadrack Makombe.

Mwangwala alisema wajumbe watano wa mkutano mkuu wa CCM Taifa walioibuka kidedea ni Charles Mwakipesile, Hamis Koko, Shadya Mtoro, Christina Gwimile na Frank Mahemba.

WILAYA YA CHUNYA.

CHAKUPEWA Makelele amefanikiwa kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Chunya baada ya kumshinda mpinzani wake mkubwa Noel Chiwanga.

Makelele alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 785, huku mpinzani wake Chiwanga akimsogelea kwa karibu kwa kuambulia kura 716.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Ileje, Rosemary Sanyamule, alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri licha ya kuchelewa kuanza kutokana na ajali iliyosababisha kifo cha kada wa CCM, Issaya Nchimbi (45), aliyefariki dunia baada ya gari alilokuwemo kupindukia mtaroni.

Rosemary alisema Naibu Waziri wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo, Philipo Mulugo, aliibuka kidedea katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC),kwa kupata kura 1034 huku wapinzani wake Polcap Ntapanya akipata kura 314, wakati Hamadi Juma aliambulia kura 96.

Katika nafasi ya wajumbe wawili wa mkutano mkuu wa CCM mkoa, waliochaguliwa ni Edina Mwangoka na Frank Chonya.

Rosemary alisema wajumbe kumi wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya waliochaguliwa ni Damson Nthangu, Antigon Kavishe, Edina Mwangoka, Anyangile Mwaipungu, James Mwanitenga, Bruno Mbegeze, Zaituni Sembo, Remji Sasun, Phide Mwalukasa na Wankunda Bangubangu.

Wajumbe watano wa mkutano mkuu wa CCM Taifa walioibuka kidedea wilayani Chunya ni Mkuu wa wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, Sauli Mwaisenye,  Polcap Ntapanya, Frank Chonya na Sophia Mwanauta.

WILAYA YA MOMBA:-
JUMA Rashid ameibuka kidedea katika nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya mpya ya Momba baada ya kuwashinda wapinzani wake wawili waliojitokeza kugombea nafasi hiyo.

Rashid alipata kura 333 akifuatiwa na Antony Mayega aliyepata kura 254 huku Nebath Simbeye akiambulia kura 245.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mwanaidy Mgogo, alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri licha ya kuwa nusura uingie dosari baada ya wajumbe kuanza kugonga madirisha baada ya kuchelewa kutangazwa kwa matokeo.

Mwanaidy alisema mjumbe wa NEC aliyechaguliwa ni Jackson Mbwile kwa kupata kura 338, akiwaacha Leonard Simbeye aliyejizolea kura 236 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Fotunartus Simfukwe aliyepata kura 189.

Aliongeza wajumbe watano waliochaguliwa katika nafasi ya mkutano mkuu wa CCM Taifa ni Mkuu wa wilaya ya Momba, Abiudy Saideya, Dr.Luka Siyame, Aden Mwakyonde, Zainabu Siame na Joina Siame.

Kwa nafasi za wajumbe wawili wa mkutano mkuu wa CCM mkoa, wagombea Fatuma Gingo na Yasinta Tung;ombe, walikuwa hawana upinzani baada ya kupita bila kupingwa.

Mwanaidy alisema wajumbe kumi wa halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Momba walioibuka kidedea ni Jeremia Msukwa, Benedicto Magai, Francis Simbeye na Erick Mkamba.

Wengine ni Sephania Msongole, Green Sichona, Luka Sikaponda, Leonard Simbeye na Daud Siwale.
...

Post a Comment

 
Top