Menu
 

Na.Angelica Sullusi.
HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imewaondoa hofu wakazi wake wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) kuwa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi ARVs zilizosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini hazikuingia Mkoani Mbeya.
 
Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, DK. SAMWEL RAZARO ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya kilichoketi hivi karibuni mjini hapa.
 
Razaro alikuwa akijibu swali la Diwani wa kata ya Isyesye, SANKE SESO ambaye alitaka kujua kama kuna madhara  yaliyowapata wakazi wa Jiji la Mbeya baada ya kubainika kuwa zipo dawa za ARVs ambazo ni bandia.
 
DK.RAZARO  amesema kuwa baada ya kubainika kuwa kuna dawa za bandia zimeingizwa sokoni, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa kushirikiana na Wakala wa usambazaji dawa nchini (MSD) walifanya ukaguzi kwa kupitia dawa zote na kugundua kuwa dawa hizo hazikuingia katika mikoa ya Mbeya na Rukwa.
 
Akizungumza na BOMBA FM baada ya kumalizika kwa kikao hicho, DK. RAZARO amesema kuwa taarifa za kuwepo kwa dawa za bandia za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi zilionyesha kuwatia hofu kidogo watumiaji ingawa hazikuathiri mahudurio ya watumiaji kwenye vituo vya kutolea dawa hizo.
 
Sakata la uwepo wa dawa za bandia sokoni tayari limeshasababisha baadhi ya maofisa wa MSD kuwajibishwa ambapo Mkuu wa MSD na viongozi wengine wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa suala hilo.

Post a Comment

 
Top