Menu
 

* Ni mchungaji wa Kanisa.
* Wawili wagunduliwa na Ujauzito
* Mmoja ashindwa kufanya mtihani.

Habari kamili na Ezekiel Kamanga,Mbozi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ipapa, Kata ya Ipunga, Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya Bwana Eliezeli Nyalutogo Kyando,anatuhumiwa kuwapa mimba wanafunzi wawili wa darasa la saba wa shule hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo Bwana Amosi Silwimba, alipokuwa akitoa maelezo katika Kituo cha Polisi cha wilaya hiyo, baada ya suala hilo kushindwa kupatiwa ufumbuzi katika kikao cha Bodi ya shule hiyo hivi karibuni.

Imedaiwa katika kikao hicho mwalimu huyo kwa nyakati tofauti aliwapa mimba wanafunzi hao, ambapo mmoja alikuwa na mimba ya miezi sita na mwingine miezi mitatu hivyo kupelekea binti mmoja kushindwa kufanya mtihani wa Taifa uliofanyika mwezi Septemba mwaka huu(Majina yamehifadhiwa).

Aidha Mwalimu Mkuu Kyando,amedaiwa kuwa ni Mchungaji mwandamizi wa kanisa moja la Kipentekoste (jina linahifadhiwa) lililopo Kata ya Ihanda wilayani humo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo na viongozi wenzake walipata malalamiko kutoka kwa wazazi wa wanafunzi hao baada ya kuonesha mabadiliko ya kimaumbile na walipo wadadisi walidai kuwa mwalimu huyo ndio mhusika, na mmoja alidai kuwa alikuwa akimpikia chakula nyumbani kwake na kutendewa ukatili huo kwa kushirikiana kimapenzi kwa awamu tatu na kumpa ujauzito ambao una miezi sita.

Kwa uapnde wake Afisa Elimu wa Shule za msingi wilayani humo amesema kuwa suala hilo lipo juu ya uwezo wake hivyo mwenye kutolea majibu ni Mwajiri ambaye ni Mkurugenzi wa Wilaya.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Bwana Leison Chilewa, amesema kuwa taarifa hizo bado hazijamfikia na kwamba yupo nje ya Ofisi na kuahidi kulifuatilia.

Post a Comment

 
Top