Menu
 

*Serikali lawamani kwa kuchelewa kutoa majibu.
*Shule Mbili zajengwa wananchi wapingana.
*Mwekezaji na wanakijiji wote kumwona Waziri Mkuu.

******
Habari na Ezekiel Kamanga,Mbarali.
Meneja Mkuu wa Shamba la Kapunga Rice Project(KRP), lililopo Kijiji cha Mapogolo, Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Bwana Wally Vermaak, amekanusha malalamiko yaliyokuwa yametolewa na wananchi wa kijiji hicho waliodai kupewa mikate yenye sumu wanafunzi wa shule ya msingi iliyopo katika uzio wa shamba hilo hivi karibuni.

Meneja huyo alikanusha shutuma hizo mbele ya Wakili wake Mheshimiwa Ladislaus Rwekaza, Oktoba 8 mwaka huu baada ya kupata taarifa ya machapisho katika vyombo mbalimbali vya habari.

Aidha Bwana Vermaak ameitaka serikali kutatua haraka mgogoro wa shamba la Kapunga na wananchi wa Mapogolo kutokana na kila upande kudai kukwamishwa kimaendeleo na kupelekea kila upande kuanza kujenga shule ya msingi wakati mwekezaji akijenga eneo la Igumbilo na wananchi wakijenga eneo la Mapogolo na mwekezaji kudai kuwa eneo hilo ni shamba lake hali inayoendelea kuchochea mgogoro uliodumu kwa takribani miaka sita mpaka sasa, huku serikali ikishindwa kutoa majibu licha ya tume mbalimbali kuundwa ili kutoa majibu halali juu ya umiliki wa mipaka.

Tume zote zimekuwa na makabrasha katika Ofisi zao na Bunge kuahidi kumaliza mgogoro huo kabla ya mwezi Agosti, baada ya swali la Mbunge wa Jimbo la Mbarali Mheshimiwa Dickson Kilufi.

Hali hiyo ya Ujenzi wa shule hizo umesababisha mpasuko wa mabishano kwa wananchi wengi wakidai shule inayojengwa na mwekezaji ni halali na wengine wakipinga shule inayojengwa na wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Ramadhani Nyoni,amedai kuwa shule inayojengwa na wananchi ipo katika uwanja wa kijiji kwa hiyo eneo hilo sila mwekezaji kama inavyodaiwa.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Gulamhussein Kifu, amesema sakata hilo alilifikisha katika ngazi ya Mkoa na Taifa hivyo hawezi kulizungumzia bali anachosubiri ni majibu kutoka Serikali kuu, pia amedai kumtaka mwekezaji kutofanya lolote juu ya kujaribu kuweka uzio katika eneo la shamba na kwamba asubiri maji u kutoka Serikali kuu.

Wakati huohuo uongozi wa Kijiji cha Kapunga umefungua madai Mahakama ya Mwanzo Chimala ukidai Mwenyekiti wa kitongoji cha Site One Bwana Ibrahimu Mwandugu anakwamisha maendeleo kwa kuzuia wananchi wake kushiriki katika ujenzi wa shule ya Msingi eneo la Mapogolo na kupelekea kumwaga maji yaliyokuwa yatumike katikaujenzi Oktoba 6 mwaka huu na kufanya uharibifu wa mifuko minne ya saruji.

Kesi hiyo imefunguliwa kwa jalada CH/PR/KUMB.30/2012 na kusomwa katika mahakama ya mwanzo Chimala Oktoba 10 mwaka huu ambapo Diwani wa kata ya Itamboleo Bwana Lwitiko Mwaipungu aliomba shauri hilo kuondolewa mahakamani hapo ili likajadiliwe kijiji kwa kuwa ni suala la kimaendeleo, na yeye ni msimamizi mkuu wa shughuli za maendeleo katika kata na mahakama iliridhia ombi hilo.

Katika hali hiyo inayoonekana kukerwa kwa muda mrefu na mgogoro baina ya mwekezaji na wanakijiji cha Kapunga pande hizo zimekubaliana kumwona waziri mkuu baada ya tume zote zilizoundwa kutatua mgogoro wa kapunga kushindwa kutoa majibu.

Hayo yalibainishwa katika mkutano uliofanyika katika Ofisi ya kijiji, ambapo upande wa mwekezaji uliwakilishwa na Afisa uhusiano Bwana Felix Mvamba, na kwa upande wa kijiji uliwakilishwa na mwenyekiti wa kijiji Bwana Ramadhani Nyoni.

Kwa pamoja pande zote mbili zimedai kuwa zinashindwa kafanya shughuli za maendeleo kwa kuwa hakuna upande ambao unaelewa mipaka yake vilivyo huku mwekezaji akidai kuwa eneo la kijiji ni eneo lake.

Post a Comment

 
Top