Menu
 

Na Solomon Mwansele, Mbeya..
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, ameibuka kidedea katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya Ujumbe Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM), wilaya ya Rungwe.

Profesa Mwandosya alifanikiwa kuwaacha kwa mbali wapinzani wake wawili waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Mkuu wa wilaya ya Kyela, Magareth Mahenga, akitangaza matokeo hayo, alisema Profesa Mwandosya ameibuka mshindi katika nafasi ya NEC kwa kupata kura 1,118.

Kada maarufu aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo, Richard Kasesela, alijikuta akiambulia kura 198 huku, Asobenye Mwandiga, ambaye naye aliingia katika kinyanyiro hicho cha nafasi ya NEC akijikuta akiambulia kura 28.

Kwa mujibu wa Magareth jumla ya kura za wajumbe walioshiriki uchaguzi huo mkuu wilaya ya Rungwe walikuwa 1,344 ambapo kura halali zilikuwa 1,354 wakati kura 12 ziliharibika.

Magareth alisema nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, imenyakuliwa na Ally Mwakalindile kwa kupata kura 948, akiwatupa pembeni wapinzani wake Samwel Mwakyambiki aliyepata kura 469 huku Antony Mwanjejele akipata kura 44.

Nafasi za wajumbe kumi wa halmashauri Kuu ya CCM wilaya zilichukuliwa na Esther Mwakipesile, Richard Kasesela, Burton Mwakasendo, Isabela Mwambela, Hawa Abdul, Amon Angetile, Twalim Mwaijumba, Michael Pascal, John Mwakifuna na Rapael Ngeko.

Aliwataja wajumbe wawili wa mkutano mkuu wa CCM mkoa waliochaguliwa kutoka wilaya ya Rungwe kuwa ni Dorith Kimambo na Michael Pascal.

Katika nafasi za wajumbe watano wa mkutano mkuu wa CCM Taifa, waliochaguliwa ni Salome Mwakalinga, Richard Kasesela, Lutengano Mwalwiba, Petro Pareso na Meckson Mwakipunga.

Wakati huo huo  Bwana Mathayo Mwangomo, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Mbarali baada ya kuwashinda wapinzani wake wawili waliokuwa wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mwangomo alifanikiwa kuibuka kidedea katika nafasi hiyo kwa kupata kura 541, na kuwashinda Ignas Mgao aliyepata kura 429 huku Benedict Masuvha akiambulia kura 76.

Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo, Florence Kyendesya, alisema jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa ni 1,080 wakati kura halali zilikuwa 1,046 ambapo jumla ya kura zilizoharibika zilikuwa ni 34.

Nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), ilichukuliwa na Geofrey Mwangulumbi kwa kupata kura 596 akiwashinda wapinzani wake Paul Kitha aliyepata kura 261 huku Hanji Godigodi akiambulia kura 137.

Florence aliwataja wajumbe wawili wa mkutano mkuu wa CCM mkoa waliochaguliwa kuwa ni Bruno Mgumba na Martin Mdenye.

Mkuu wa wilaya ya Mbarali, GullamHussein Kifu, aliongoza kwa kupata kura nyingi katika nafasi za wajumbe weatano wa mkutano mkuu wa CCM Taifa, na wengine waliochaguliwa ni Yusuph Mwaipalu, Muhenza Mlwilo, Salome Stemile na Feinti Mwashikumbulu.

Kwa upande wa nafasi kumi za wajumbe wa halmashauri Kuu ya CCM wilaya walioibuka kidedea ni Zamoyoni Mhanji, Hanji Godigodi, Amadi Njolombe, Defesi Kihombo na  Ambindwile Mwaijumba.

Wajumbe wengine waliochaguliwa katika nafasi hiyo ni Eliud Mahenge, Feinti Mwashikumbulu, Cliford Mwakiholano, Abdul Mulla na Jeremiah Kadenge.

Post a Comment

 
Top