Menu
 

NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.

UCHAGUZI wa nafasi ya Katibu,Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Mbeya mjini, unatarajiwa kurudiwa upya Oktoba 2, mwaka huu baada ya wagombea kushindwa kufikia nusu ya kura zilizopigwa.

Imeelezwa kwa mujibu wa Katiba, watakaorudia kuchuana ni wagombea wawili waliopata kura nyingi katika mchuano wa kwanza huku jina la mgombea wa tatu likiondolewa.

Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya mjini, Raymond Mwangwala, akizungumza na Uhuru jana alisema wagombea watatu walijitokeza kuwania nafasi hiyo na kura zao walizozipata zikiwa kwenye mabano, ni Dk.William Mwamakimbula (78), Dk.Robert Mgazwa (09) na Hussein Lutelo (77).

Alisema katika uchaguzi huo, uliofanyika ukumbi wa CCM mkoa wa Mbeya, jumla ya wajumbe 164 walishiriki hivyo mshindi alitakiwa kupata kura zaidi ya nusu ambazo ni 83.

"Hivyo kutokana na wagombea wawili wa kwanza kushindwa kupata nusu ya kura kwa mujibu wa Katiba, uchaguzi huu utarudiwa tena Oktoba 2, mwaka huu ili tuweze kumpata mshindi halali" alisema Mwangwala.

Kwa mujibu wa Mwangwala, mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo Dk.Mgazwa alilazimika kukimbizwa hospitali ya Rufani Mbeya, baada ya kupatwa na homa kali ambapo alilazwa na hali yake kwa sasa inaendelea vizuri.

Aliongeza katika nafasi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wilayani humo, jumla ya wanachama kumi na sita walijitokeza lakini waliofanikiwa kushinda ni Charles Mwakipesile, Edina Mwaigomole, Fatuma Kasenga na Godfrey Habaya.

Mwangwala alisema mmiliki wa kituo cha redio cha Sweet Fm kilichopo mjini Mbeya, Emmanuel Mbuza, alifanikiwa kuibuka kidedea katika nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi wilayani humo.

Aliongeza Mbuza alipata kura 112 na hivyo kuwatupa kando wagombea Philimon Mung'ong'o aliyepata kura 46 huku Stephan Gwimile akiambulia kura kutoka kwa wajumbe sita.

Post a Comment

 
Top