Menu
 

Na Ester Macha,
 WAKULIMA wadogo wanaojishughulisha na kilimo cha Mpunga Mkoani Mbeya wamepata ufadhili wa kusaidiwa mashine za kisasa za kukobolea mpunga ambazo watakuwa wanazilimiliki wenyewe ili kuboresha kilimo chao na kuachana na mbinu za kizamani.

Ufadhili huo wa mashine wameupata kutoka Kampuni ICM ya Australia baadaya kampuni hiyo kuvutiwa na harakati za Kampuni ya Mtenda Kyela Rice katika kusaidia wakulima wadogo wa kilimo cha mpunga Mkoani hapa.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Mtendaji wa wa Kampuni hiyo Bw.Douglas Shears aliyefuatana na mkewe Deirdra Shears wakati alipotembelea kampuni ya Mtenda ambayo inasaidia wakulima wadogo Mkoani hapa.

Alisema  kuwa kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na kampuni ya Mtenda kuanzisha mradi kama huo  uliopo Kigali, kusaidia wakulima wa mpunga kumiliki  mashine zao ya kisasa  kwa wakulima wadogo waliopo katika wilaya mbali mbali ambazo zinalima mpunga.

"Natambua kuwa baada ya kupata mashine hizi za kisasa wakulima watakuwa na pembejeo, mbinu bora za kilimo na kukuza masoko ya ndani kwa kumlenga mlaji mwenye uwezo mdogo bila kusaidia soko la nchi zinazopakana na Mbeya"alisema.

Bw. Shears aliendelea kusema kwamba taarifa za Mtenda Kyela Rice amezipata kutoka kwa Melinda & Bill Gates Foundation huko nchini Marekani kwamba akitaka kufanya biashara  ya mpungaTanzania basi hana budi kukutana na Bw.George Mtenda ambaye anafanya biashara hiyo kwa mafanikio makubwa.

"Nitaandika andiko kwenye kikao cha bajeti cha ICM Australia cha Februari 2013 nina uhakika wa kupata baraka zote za bodi ili utekelezaji wake  uanze mara moja na kwamba imepita takriban miezi miwili toka asasi ya Melinda & Bill Gates

Foundation kutoka Marekani kuonyesha nia ya kusaidia wakulima wa mpunga Nyanda za Juu kusini kupitia kampuni ya Mtenda Kyela Rice Co. Ltd "alisema.

Akiwa katika kikao cha pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mtenda Bw.George Mtenda, Emile Malinza (Mshauri wa kampuni) na Jesko Linga ambaye ni Afisa Kilimo wa kampuni, Bw.Shears alisema nia yao ya
kufanya biashara Tanzania tayari wameshafungua kampuni yao Dar es Salaam inayojulikana kama ICM Tanzania na kwamba mipango iko mbioni kununua mashine ya kukoboa mpunga ya sh.200,000,000 na kusindika kahawa tayari kuanza kazi.

Pia alisema kuwa tayari wameshafungua kampuni kubwa Kigali, Rwanda ya kuendeleza kilimo cha mpunga na wakulima 30,000 wameshaanza kufaidi matunda ya uwekezaji huo.

Baada ya mazungumzo hayo Mkurugenzi wa Kampuni ya mtenda Rice Bw.George Mtenda alimpeleka mwenyeji wake katika kiwanda cha Wella Mills, cha  kukoboa mpunga  cenye  uwezo ya kuchambua uchafu na kupanga mchele kwenye madaraja mbalimbali .


Aidha Bw. Mtenda alisema kampuni yake ina wakulima zaidi 15,000 ambao wapo Wilaya ya Kyela na Momba na Kamsamba  ambao wanajishughulisha na kilimo cha mpunga na kusema kuwa mashine hizo wakulima wanatarajiwa kuzipata mara baada ya kikao cha bajeti cha Australia kuisha mwezi januari.

Post a Comment

 
Top