Menu
 MKUU wa mkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma.


MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita wameishambulia halmashauri ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wakidai baadhi ya watendaji wake wamekithiri kwa ubadhilifu.

Wakati Mkuu wa Mkoa akidai kwamba halmashauri hiyo ina kashfa nzito za ubadhilifu, Mkuu wa Wilaya alisema makundi ya kisiasa wilayani humo yanawachochea baadhi ya watendaji kufuja fedha za halmashauri hiyo.

Katika ziara yake aliyoifanya juzi kugagua shughuli za maendeleo na kuhamasisha kilimo, Dk Ishengoma alisema vitendo hivyo ambavyo hata hivyo hakuvitaja kwa madai ya kutoingilia vyombo vya sheria, vinautia aibu mkoa wa Iringa.

Aliiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya  wilaya hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuongeza kasi ya kufuatilia matumizi ya fedha za halmashauri hiyo ili kuisafisha kutoka mikononi wa wabadhilifu.

“Tumepewa meno, Mkuu wa Wilaya anaweza kuchukua hatua kali pale anapoona mambo hayaendi sawa, lakini pia Chama cha Mapinduzi kina wajibu mkubwa wa kuangalia jinsi watendaji wa serikali wanavyotekeleza Ilani huku wakionanisha ubora wa kazi na thamani ya fedha zinazotumika,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kusimamia fedha za serikali na kumuonya asimvumilie mtendaji yoyote anayefanya ubadhilifu.

“Msiibe hata kama mishahara yenu mnaona haitoshi, nyinyi ni sehemu ya jamii kwahiyo ni muhimu baada ya kazi mkafanya shughuli zingine za maendeleo kama kilimo, kufuga na zinginezo,” alisema.

Mbele ya baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo, kwa upande wake Mkuu wa Wilaya alisema amejifunza mengi sana katika kipindi cha miezi sita tangu awe mkuu wa wilaya hiyo.

Guninita alisema wilaya ya Kilolo inakabiliwa na changamoto kubwa ya makundi ya kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kuwagawa watendaji wa halmashauri hiyo.

“Makundi hayo yanasababisha ubadhilifu mkubwa ndani ya halmashauri hiyo kwa lengo la kukomoana kisiasa,” alisema.

Alisema kashfa za baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo kujihusisha katika vitendo vya kifisadi zitamalizwa kwa kumaliza makundi ya kisiasa ambayo hata hivyo hakuyataja.

Baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo walipoulizwa kuhusiana na madai hayo walikataa kutoa ufafanuzi kwa kile walichodai kwamba Takukuru inaendelea kuwachunguza baadhi yao.

Wakati hayo yakitokea, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana  UVCCM) wa wilaya hiyo, Sifuni Mwakongwa amewataka vijana wa umoja huo kutumia nguvu zao zote kukataa kupokea miradi inayotekelezwa chini ya kiwango ndani ya wilaya hiyo.
 

Post a Comment

 
Top