Menu
 

Na Esther Macha, Mbarali
Sakata la matumizi mabaya ya shilingi bilioni 2.2 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, limechukua sura mpya baada ya baraza la Madiwani kuamuru ufanyike ukaguzi maalumu ili kubaini wahusika  na waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Hatua hiyo imetokana na kamati ya fedha , uchumi na Mipango ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwasilisha taarifa ya uchunguzi , kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abas Kandoro kutoa miezi miwili kwa Halmashauri hiyo kuweka sawa hesabu zao.

Agizo hilo lilitolewa jana na madiwani hao,  katika kikao cha kawaida cha kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo za kata kwa robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2011/ 2012 , kilichofanyika katika ukumbi wa Bomani Mjini Rujewa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya fedha, uchumi na mipango wa Halmashauri hiyo,Bi. Guzza Sabri kuwasilisha taarifa ya utekelezaji, ikiwemo taarifa ya sakata la matumizi mabaya ya kiasi hicho cha fedha, ndipo madiwani wenzake waliibuka na kupinga na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Adam  Mgoyi ndani ya wiki mbili awe amwemwita mkaguzi  na mdhibiti  mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu juu ya tuhuma hizo za matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo zinazowakabili baadhi ya wakuu wa idara.

Akizungumza katika kikao hicho Diwani wa kata ya Mswiswi Bw. Frugence Muhegele alisema kwamba miezi mwili yote ambayo kamati ya fedha   na mipango ilipewa jukumu la kufanya kazi hiyo imeshindwa kusema chochote mpaka sasa na kuomba  nguvu nyingine halmashauri  iongoze nguvu.

Diwani huyo alisema kuwa hakuna diwani ambaye  hana uchungu wa fedha za miradi ya maendeleo ambazo zinatolewa  kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi ambayo mpaka sasa imesimama kutokana na kutokuwa na fedha za ukamilishaji na  miradi mingine iliyokuwa inaanza  kujengwa .

 “Sisi tunataka  ufanyike uchunguzi wa kina kuhusu fedha hizi ili wahusika waweze kubainika na kuchukuliwa hatua za kisheria  mmoja baada ya mwingine , kwani kitendo hiki si kizuri na suala hili la ubadhilifu limekuwa la muda mrefu bila kubaini nani mhusika halisi aliyehusika hivyo ni vema mkaguzi na mdhibiti aje afanye kazi hii mapema”walisema madiwani hao.

Akijibu hoja za madiwani hao Mwenyekiti wa hamlashauri ya wilaya ya Mbarali Bw. Keneth Ndingo aliwataka madiwani  kuwa na subra kwa kufuata sheria  na kumsubiri mkaguzi na mdhibiti  mkuu wa hesabu za serikali aje kufanya kazi yake ,majibu ya (CAG) ndo yatatotoa jibu sahihi na kubaini wahusika halisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Bw. Adam Mgoyi alisema kuwa tayari ameongea na  Mkaguzi  mkazi  kwamba wiki ijayo anakuja kufanya ukaguzi huo haraka halmashauri kuhusiana na fedha hizo .

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro katika kikao chake na madiwani na wakuu wa idara  alisema fedha hizo zinaonekana kuandikiwa taarifa ya matumizi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini Halmashauri hiyo imeshindwa kuweka viambatanisho ili kuthibitisha uhalali wa matumizi na thamani  halisi kati ya fedha iliyotumika na miradi uliotekelezwa.

Alisema taarifa hiyo ya mabilioni hayo kukosa nyaraka na viambatanisho ni ya mwaka wa fedha ulioishia juni mwaka huu na si ya (CAG), na kwamba upungufu huo ambao unakiuka taratibu za fedha umegunduliwa kamati ya fedha na uchumi ya mkoa, iliyoketi hivi karibuni na kupitia taarifa kutoka Halmashauri zote za mkoa wa Mbeya.

Kutokana na hali hiyo Bw. Kandoro alitoa miezi miwili kwa watendaji hao wawe wamewasilisha taarifa mpya ikiwa na viambatanisho , tofauti na hapo hatua kali zitachukuliwa kwa wote walishindwa kutimiza wajibu wao, ikiwemo kupendekeza halmashauri kufutwa.

Post a Comment

 
Top