Menu
 

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mwanamke mmoja aliyetambulika kama Jenista Mapunda (24) mkazi wa Mfaranyaki mjini Songea amejifungua mtoto kisha kumnyonga na kumzika yeye mwenyewe alfajiri ya siku ya Jumapili (jana) katika makaburi ya Mfaranyaki.
Watu waliofika kushuhudia tukio hilo la aina yake walimshangaa kwa kuwa na roho ya ukatili hali ambayo pia ilimfanya kuchimba kaburi yeye mwenyewe, kumzika mwanawe na kuweka msalaba wa mti kama ilivyo desturi kwenye maziko.
Kaburi ambalo lilichimbwa na Jenista Mapunda(24) ambalo alimzika mtoto wake baada ya kujifungua kisha kumzika na kuweka msalaba yeye mwenyewe
 
Kalista Kifaru(38) mkazi wa Mfaranyaki aliifahamisha FikraPevu kuwa majira ya saa 12 alfajiri aliambiwa na mtoto wake ambaye alipita eneo la makuburi kwamba amemuona mwanamke analia amelala juu ya kaburi  ndipo alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa wa Mfaranyaki ndugu Gabriel Ndewele.
 
Mwenyekiti huyo wa mtaa akiwa pamoja na baadhi ya wakazi wa Mfaranyaki walikwenda katika eneo la tukio ambapo walimkuta Jenista akiwa ameishiwa nguvu kutokana na kutokwa na damu nyingi.
 
Alipohojiwa Jenista alidai kuwa ni kutokana na ugumu wa maisha ndiko kulimpelekea alipojifungua karibu na vyoo vya shule ya msingi Misufini kuamua kumnyonga mtoto wake hadi kufa kisha kumbeba na kwenda kuchimba kaburi na kumzika kwenye makaburi ya Mfaranyaki.
Jenista Mapunda(24) akiwa katikati ya polisi wawili ambao walimkamata baada ya kudaiwa kumzaa mtoto, kumnyonga kisha kumzika yeye mwenyewe katika makaburi ya Mfaranyaki mjini Songea
 
“Nilipojifungua niliamua kumnyonga kubeba maiti kuchimba kaburi mimi mwenyewe kisha kumzika, nilizidiwa peke yangu niliishiwa nguvu kutokana na kutokwa na damu nyingi, niliamua kulia na kulala juu ya kaburi la mtoto wangu”, alisema.
Polisi wakiwa katika makaburi ya Mfaranyaki mjini Songea kufuatilia tukio la Jenista Mhagama kudaiwa kumnyonga mtoto wake na kumzika
Polisi wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambapo hivi sasa wanamshikilia mwanamke huyo kwa upelelezi na uchunguzi zaidi. Hata hivyo mwanamke huyo amepelekwa kupatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma na hali yake inaendelea vizuri.
Habari hii imeandikwa na Albano Midelo, FikraPevu – Songea

Post a Comment

 
Top