Menu
 

Na Esther Macha,
KWA Mkoa wa Mbeya zao la Mpunga  limekuwa  likilimwa katika maeneo mbali mbali kutokana na ardhi ya Mkoa wa Mbeya kukubali  zao  hilo kwa kiasi kikubwa ,na  kuwa mkombozi kwa mkulima mdogo hasa wa vijijini kwa kuwaingizia kipato kikubwa katika familia  na hivyo kuondokana na hali  duni ya kimaisha.


Lakini   ili zao hilo liweze kupewa kipaumbele hakuna budi kwa wakulima kupatiwa mbegu bora  pamoja mbolea ambayo itafanikisha kupata  mazao yaliyo bora ili kuwawezesha kupata masoko ya  uhakika  nje ya nchi .


Katika  hili serikali inawajibu wa kuhakikisha kuwa wakulima waliopo vijijini wanapewa kipaumbele kwa kupatiwa mbegu bora pamoja na mbolea kwa wakulima hao ili waweze kuzalisha mpunga  wenye kiwango ambao utakuwa msaada kwao kwa kupata masoko yenye uhakika.


Ili kuhakikisha kuwa  wakulima waliopo vijijini wanalima mazao  ambayo yanakuwa na ubora hususani zao la mpunga baadhi ya kampuni tayari zimeanza kujitokeza kusaidia wakulima  wanaojishughulisha na kilimo cha mpunga kuwapatia mbegu bora na mbolea ili waweze kuboresha mazao  yao.


Hivi karibuni Kampuni ya Mtenda Kyela Rice Co. Ltd  iliyopo Mkoani Mbeya  imekuwa msaada mkubwa  kwa wakulima wa zao la mpunga wa nyanda za juu kusini .

Ili kufanikisha juhudi za wakulima kampuni hiyo imedhamilia kuwainua wakulima wa zao la mpunga waliopo vijijini na mjini  kwa kuwa na mpunga wenye hadhi ambao watauza kwa masoko ya nje.


Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni Mkurugenzi  wa kampuni hiyo Bw.George Mtenda anasema kuwa kampuni hiyo ilianzishwa  mwaka 2006 kwa lengo la kununua mpunga  na kuwaelimisha wakulima  kwa kutoa elimu bora ili waweze  kuzalisha mazao yenye ubora.


“Kupitia kampuni hii tunataka kuhakikisha kuwa wakulima wanazalisha mpunga wenye kiwango cha juu  ambao utawanuisha  kwa kuwa na kipato kizuri katika familia zao  kwa kutoka waliopo sasa  na kusonga mbele”anasema Bw. Mtenda.


Anasema kuwa wakulima walio wengi kwa muda mrefu wamekuwa wakijishughulisha na kilimo  kisichokuwa na tija kutokana na kutokuwa na elimu  kwa kulima mazao yao ili mradi bila kujiwekea malengo yeyote pale wanapolima.


Hata hivyo Mkurugenzi huyo anasema kuwa  wakulima wadogo waliopo vijijini  pamoja na kuwapatia elimu hiyo pia  kama kampuni wamekuwa wamekuwa na utaratibu wa kuwapatia  mbegu  bora  kwa kuwakopesha  kwa grama ndogo  ambayo wanamudu  wakulima hao kutokana na maisha ya kijijini yalivyo.


Anasema kuwa  wakulima wadogo waliopo vijijini wanahitaji msaada mkubwa wa kupatiwa elimu juu ya kilimo chenye tija ili waweze kuondoka walipo sasa vinginevyo wakiendelea na kilimo cha kizamani hawataweza kufika popote  hivyo ni vema  makampuni yanayojihusisha na masuala ya kilimo kusaidia wakulima.


Wakulima hao baada ya kupata elimu hiyo kutoka kampuni hiyo nao kama umoja wao wa wakulima wadogo huenda vijiji vya jirani kuwapatia mbegu bora za mpunga ili nao waweze kuzalisha  mpunga mzuri ambao utaweza kuwapatia soko zuri.


Hata hivyo anasema kampuni ya Mtenda ina wakulima zaidi ya 14,600 kwa mkoa wa mbeya  na ambao wanapata huduma kutoka kampuni hiyo.


“Kutokana na elimu hii ambayo kampuni inatoa pamoja na kuwakopesha wakulima mbolea kwa kila mkulima anazalisha gunia 100  mpaka 150 kwa heka haya ni matumaini mazuri kwetu ambayo sasa yanazaa matunda mazuri kwa wakulima  hawa”anasema.


 Bw. Mtenda anasema kampuni hiyo imekuwa ikisaidia wakulima wa, Kamsamba, Momba pamoja na Kyela  ambao mpaka sasa wameonyesha kuwa na mafanikio kwa kuachana na kupanda mbegu zisizokuwa na ubora wowote.


Anasema kuwa baada ya kukopeshwa  mbolea hizo wakulima hurudisha mpunga baada ya mavuno na na mbegu kwa kulipia grama ndogo ambayo ni rahisi kwa mkulima wa kijijini kuweza kumudu kulingana na maisha ya mtu  mwananchi kijini wa kuwa na kipato duni.


Mmoja wa wakulima wa zao la mpunga ambao wameweza kunufainika kupitia kampuni ya Mtenda Bi. Neema Simbeye mkazi wa Momba  anasema kuwa kupitia kampuni hiyo ameona mafanikio  makubwa katika kilimo hicho kwani awali wakati anaanza kulima mpunga alikuwa akizalisha kwa heka moja gunia  5 ambayo kwa sasa imevuka sana.


“Mimi kama mwanamke lazima niseme ukweli kuhusu kampuni hii , mimi kwa upande wangu nashukuru sana kwani kwa sasa navuna zaidi ya gunia 100 kwa heka na vile vile kutokana na mafanikio haya nimeweza kusomesha watoto wangu na mahitaji mengine ya kifamilia ambayo awali yalikuwa changamoto kubwa katika familia yangu.


Hivi karibuni Kampuni ya ICM ya Australia baada ya kuona mafanikio ya kampuni ya Mtenda Rice iliamua kumtuma Mwenyekiti  Mtendaji wake Bw.Douglas Shears kuangalia utendaji wa kampuni hiyo.


Akiwa katika mazungumzo hayo ya kibiashara  Bw. Shears anasema kwamba yeye ametoka Melbourne, Australia kuja Mbeya kuonana na George Mtenda kuhusiana na kufanya kazi pamoja katika kilimo cha mpunga nyanda za juu kusini kwa pamoja ili kuweza kuwasaidia wakulima wadogo waliopo vijijini.


Hata hivyo Bw.Shears aliendelea kusema kwamba taarifa za Mtenda Kyela Rice amezipata kutoka kwa Melinda & Bill Gates Foundation huko Marekani kwamba akitaka kufanya biashara  ya mpunga Tanzania.


Bw. Shears anasema kuwa kuonesha nia yao ya kufanya biashara Tanzania tayari wameshafungua kampuni yao Dar es Salaam inayojulikana kama ICM Tanzania na kwamba mipango iko mbioni kununua mashine ya kukoboa mpunga ya Shilingi 200,000,000  ya kusimikia kahawa tayari kuanza kazi.


Aidha  Mkurugenzi huyo  anasema nchini Kigali Rwanda wameshafungua kampuni kubwa ya  kuendeleza kilimo cha mpunga na wakulima 30,000 wameshaanza kufaidi matunda ya uwekezaji huo.


Hata hivyo Bw. Shears anasema amevutiwa na harakati za kampuni ya Mtenda  ya kusaidia wakulima wadogowadogo wa  mpunga na kuhaidi kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana na kampuni ya Mtenda kuanzisha mradi kama uliopo Kigali, kusaidia wakulima wa mpunga kumiliki mashine zao za  kisasa za kukobolea mpunga.


Anasema kuwa  mashine hizo kwa wakulima wadogo ni kuboresha kilimo kwa usambazaji wa pembejeo, mbinu bora za kilimo na kukuza masoko ya ndani kwa kumlenga mlaji mwenye uwezo mdogo bila kusaidia soko la nchi zinazopakana na Mbeya.


Aidha Mkurugenzi huyo ameahidi kupeleka andiko kwenye kikao cha bajeti cha ICM Australia cha Februari 2013 ili utekelezaji wake uweze kuanza mara moja  Aprili 2013.


Bw. Shears  baada ya kutembelea ofisi ya Mtenda iliyopo eneo la Soweto Jijini  Mbeya alipata muda wa kutembelea kituo cha uwekezaji kanda ya nyanda za juu kusini  (TIC) kwa lengo la kuonana na Meneja wa  wa kituo hicho Bw.Daudi Riganda  ambaye alihaidi kuwa ofisi yake itampa ushirikiano wa kutosha.


Bw. Riganda anasema  kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa azma ya kushirikiana na  kampuni ya mtenda katika harakati zake za  kuwakomboa wakulima  wadogo wadogo  wa mpunga .

Post a Comment

 
Top