Menu
 

 -Alitakiwa kutumikia adhabu ya mumewe aliyetuhumiwa kumuua mwanakijiji mwenzo.
 -Polisi wamuokoa yeye na mumewe na kuwaficha kusiko julikana.

Na Moses Ng’wat,Mbeya.
MWANAMKE mmoja, Shida Hasanya, amenusurika kuzikwa akiwa hai, akitakiwa kutumikia adhabu ya mumewe aliyetoroka baada ya kutuhumiwa kuhusika kumuua mwanakijiji mwenzake kwa imani za kishirikina.

 Tukio hili ni la pili kutokea mkoani hapa, ambapo Aprili 28 mwaka huu, wananchi wa kitongoji cha Itezi Magharibi, katika kata ya Itezi, Jijini Mbeya, waliamua kumzika akiwa hai mkazi mwenzao Nyerere Kombwee, wakimtuhumu kumuua mtoto wa mdogo wake kwa imani za

Taarifa za tukio hilo ziliibuliwa juzi na Diwani wa viti maalumu, Veronika Mzumbwe (CCM), wakati akitoa ushahidi wa kisa mkasa katika maadhimisho ya kongamano la kutafakari siku 16 za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na yanatarajia kuhitimishwa leo.

Akitolea ufafanuzi zaidi diwani huyo, alisema kuwa tukio hilo ambalo lilimtokea mwanamke huyo baada ya mumewe kutoroka, lilitokea Disemba 5 mwaka huu, katika kitongoji cha Ihenga, kata ya Isuto wilayani Mbeya Vijijini.

Alisema maamuzi hayo ya wanakijiji yalifikiwa baada ya mume wa mwanamke huyo, Shila Njela, ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, kudaiwa kutoroka baada ya kutuhumiwa kuhusika na kifo cha mwanamke mmoja kijijini hapo aliyetajwa kwa jina la Sala Maisha (Mama Hawa) .

Inadaiwa kuwa marehemu Mama Hawa alikufa katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuibuka ugomvi kati yake na Mwenyekiti wa kijiji hicho, ugomvi unaosadikiwa kusababishwa na biashara ya Samaki.

Ilielezwa kuwa siku chache kabla ya mwanamke huyo kufariki, inadaiwa kuwa Mwenyekiti huyo alifika nyumbani kwa marehemu na kununua Samaki, lakini katika hali ambayo haikueleweka aliwarudisha Samaki hao, ndipo marehemu aligoma kuwapokea na kuibuka ugomvi.

Inadaiwa kuwa baada ya kurushiana maneno makali, siku chache baadae  marehemu huyo aliyekuwa mfanyabiashara wa samaki alianza kuumwa na kupelekwa Mjini Mbeya kwa ajili ya matibabu na baadae kufari, jambo walilomtuhumu Mwenyekiti wao kuhusika na kuamua kutaka kumzika akiwa hai badala ya marehemu.

“Wakati familia ya marehemu ikiandaa mipango ya mazishi ya ndugu yao , ikiwemo kuchimba kaburi,  kulianza kuibuka tetesi msibani hapo kuwa kundi la vijana lilikuwa limepanga  kulipiza kisasi kwa kutaka kumzika kiongozi akiwa hai kwa imani kuwa yeye ndiye aliyehusika na kifo hicho” alifafanua diwani huyo.

Aliongeza kuwa baada ya Mwenyekiti huyo kupata tetesi hizo ghafla aliamua kutoroka eneo hilo la msiba ambako alikuwa anaendelea na ukusanyaji wa fedha za michango ya msiba.

Mzumbwe alisema baada ya vijana hao kubaini kuwa mwenyekiti huyo katorokea kusiko julikana waliamsha hasira na kwenda kumfuata mke wake nyumbani, ambapo walimfanyia vurugu .

“Mwanamke yule hakuwa na namna, kwani walipombana wakiwa wamemzunguka alikiri kuhusika na vitendo vya ushirikina kwa kushirikiana na mumewe na baadhi ya watu kijijini hapo”.

Alisema baada ya maelezo hayo vijana hao walimtaka alipe kiasi cha shilingi 720,000 kama gharama za usumbufu kwa wao kuchimba kaburi la sivyo wangezika akiwa hai badala ya mumewe aliyefanya kitendo hicho na kukimbia.

“Tunashukuru  kwani wakati yote hayo yakiendelea kumbe kuna baadhi ya viongozi wa Kata hawakupendezwa na mpango huo waliamua kutoa taarifa polisi ambao walifika majira ya saa kumi wakiwa na silaha hivyo kundi hilo la vijana lilisambaratika kwa kukimbilia kusiko julikana” alisema Mzumbwe.

Aliongeza kuwa polisi kwa kushirikiana na polisi walitumia Diplomasi kuwarudisha vijana hao kwa ahadi ya kutokamatwa mtu yeyote na walikubali na kuzika marehemu majira ya saa tatu usiku.

Alisema baada ya kumaliza kusaimamia maziko hayo walimchukua mwanamke huyo aliyenusurika pamoja na mumewe ambaye alikuwa amehifadhiwa na wasamaria wema na kuondoka nao, ambapo hadi sasa hawajarudi kijijini hapo.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Diwani Athman, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi baada ya kufanikiwa kuwaokoa watu hao wamewahifadhi kwa mmoja wa ndugu, wakati wakisubiri taratuibu nyingine zaidi juu ya tukio hilo .

“Ninachoweza kusema ni kweli tukio hilo limetokea, kazi ya jeshi la polisi ni kulinda usalama wa kila raia, watu hao tuliwaokoa na kuwatoa huko na sasa tunawahifadhi mahali Fulani kwa ndugu yao…..kwani si vizuri kupataja maana huwezi juwa wale watu bado wanafikiria nini juu yao na jumatatu (yaani leo) tutaenda kukutana na wananchi hao kwa ajili ya kutoa elimu zaidi” alisema Diwani.

Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Mwenyekiti huyo ambaye hivi sasa anaishi uhamishoni kusikojulikana na kukili kukumbwa na mkasa huo, huku akiomba apewe nafasi zaidi ya kupumzika bada ya kulieleza jambo hilo kwenye vyombo vya habari.

Post a Comment

 
Top