Menu
 

 
 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kuwa fedha zote ambazo wenyeviti wa vitongoji wanaidai Serikali kama posho ya usimamizi wa zoezi la sensa ya makazi na watu zitalipwa hivi karibuni.

 

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Desemba 22, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Kibaoni kwenye uwanja wa shule ya msingi Kakuni ambako pia ni kijijini kwao akiwa katika siku ya kumi ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

 

Alikuwa akijibu swali la Bw. Wejja Hassan mkazi wa kijiji cha Kibaoni ambaye alitaka kujua ni kwa nini wao wamelipwa posho ya sh. 10,000/- wakati waliacha kazi zao na familia zao wakati wakizunguka na maofisa wa sensa.

 

Waziri Mkuu alisema wenyeviti wote waliofanya kazi kwa siku saba na wale ambao maeneo yao yaliongezwa siku za ziada watalipwa kwa sababu fedha zimeshapatikana.

 

“Serikali imeshafanya hesabu zake na tumebaini jumla ya shilingi bilioni 3.1/- zinahitajika. Fedha zimeshapatikana na zitalipwa hivi karibuni,” alisema.

 

Akijibu swali la Bw. Godwin Mbassa kuhusu kupanda kwa bei ya mahindi kijijini hapo kutokana na wimbi la viwavi jeshi, Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao kuanza kuweka akiba ya chakula kwa ajili ya familia zao mara baada ya kuvuna.

 

“Mnasema bei ya debe moja la mahindi ni shilingi 15,000/- kwa wenzenu Usevya wanauziwa shilingi 18,000/-. Tatizo la bei halikuja kwa sababu ya viwavijeshi bali ni kwa sababu ya uzalishaji mdogo msimu uliopita ama kutoweka akiba ya chakula baada ya kuvuna,” alisema.

 

“Hili ni onyo kwa wakulima, inabidi mkishavuna msiuze chakula chote kwa kuzingatia kuwa kuna wakati bei itapanda. Kwa hiyo jifunzeni kuweka akiba ya chakula ili muuze zaidi,” alisema.

 

Alisema kwa wastani kaya moja inahitaji kuweka magunia 10 -15 kama akiba ya chakula ya mwaka mzima. “Kwa hiyo mtu akivuna magunia 40 atoe akiba ya familia yake na yanayobaki auze,” alisema.

 

Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake jana (Jumamosi, Desemba 22, 2012) kwa kufanya kikao cha majumuisho ambapo alizungumza na viongozi chama na Serikali wa wilaya za Mlele na Mpanda katika shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko kata ya Kibaoni.

Post a Comment

 
Top