Menu
 

SERIKALI wilayani Mbarali Mkoani Mbeya imesema itawafikisha katika vyombo vya sheria walimu wote wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi, huku baadhi yao wakiwapa mimba na kuwageuza wake zao watoto hao wa shule.

Amesema  kuwa tabia hiyo ni uvunjaji wa maadili, na tabia ya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi ni moja ya ubakaji kwa kuwa umri wa wanafunzi hao upo chini ya uangalizi wa walezi au wazazi.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Bw. Hussein Kiffu   wakati wa mkutano wa wadau wa elimu uliofanyika wilayani hapa katika ukumbi wa Rutheran .

Aliwataka walimu wenye tabia hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani ataanza kupita katika maeneo ili kupata taarifa za wanaume wanao/waliowapa mimba wanafunzi, huku viongozi wa eneo ambao hawakuchukua hatua zozote juu ya tatizo la mimba nao kusika kisheria.

 Aidha alisema kwa kuwa walimu ni walezi wa wanafunzi,  hawatakiwi kufanya suala lolote lililo baya kwa watoto hao,  nakwa mujibu wa sheria za nchi walimu watakaokutwa na makosa ya aina hiyo ya ubakaji watafungwa miaka isiyo chini ya miaka 30.

 “Walimu wanatakiwa kuwalea vyema watoto wetu, na ili kutokomeza tatizo hilo tumeanza kwa  kila mkuu wa idara anakuwa ni mlezi wa Kata, ili kuwaelekeza wananchi juu ya wajibu wao, na watakuwa chachu ya maendeleo katika ngazi ya kata, na kwa utawala tulionao tuache kufanya kazi kwa mazoea,” Alisema Kifu.

 Akitoa taarifa ya uchunguzi katika sekta ya elimu Wilayani humo, katibu mtendaji wa asas ya kiraia ya Usangu Non Governmental Organization Network (USANGONET) Bw.Paulo Kitha alisema mmomonyoko wa maadili wa wazazi, walimu na wanafunzi ni moja ya changamoto inayokwamisha sekta ya elimu wilayani humo, huku baadhi ya walimu kutokuwa na moyo wa kujituma katika kufanya kazi yao.

Bw. Kitha alisema baadhi ya walimu wamebainika kutokuwa na uwezo wa kutosha kufundisha huku mahusiano hafifu baina ya walimu na wazazi yakitoa fulsa kwa wanafunzi kuvunja maadili ya kitanzania.

Naye mratibu wa elimu Wilaya ya Mbarali Bw.Richard Kantamba akisoma taarifa ya ya elimu, alisema kuna uwepo wa wanafunzi zaidi ya elfu 11 wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Bw.Mantamba alisema tatizo hilo linatokana na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo yaupungufu mkubwa wa walimu, uhaba wa majengo ya shule, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na samani.

Aidha mratibu huyo alisema hata utoro uliokithiri kwa wanafunzi  ni sababu ya kiwango hicho cha wanafunzi kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu, na kupelekea wilaya kutofanya vizuri katika matokeo ya mtiani wa darasa la saba.

Akitoa takwimu ya ufauru,Bw. Mtambe alisema Wilaya imekuwa ikisdhika nafasi ya mwisho katika matokeo hayo ambapo mwaka 2010 wilaya ilishika nafasi ya mwisho kimkoa, na mwaka 2011 kushika nafasi ya tano kati ya wilaya 8 za mkoa wa Mbeya.

 Mchungaji Jackob Mwabeya alisema changamoto nyingine ni pamoja na baadhi ya walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi, huku badhi ya maofisa wakiwafanyia unyama walimu wanaokataa kuhusiana nao kimapenzi.

 “Hili tatizo linatupa hasara kubwa sisi wazazi, hapa kuna matatizo mengi, kuna baadhi ya maofisa elimu wamekuwa wakiwataka kimapenzi walimu wanaotoka vyuo na baada ya kukataa viongozi hao huwahamisha na kuwapeleka shule zenye changamoto kubnwa, kwa hiyo mwalimu anakuwa hana raha, anafanya kazi kwa hofu na mashaka,” Alisema Mwabeya.

Aidha Bw.Mwabeya aliongeza kuwa tabia ya kuna walimu ambao wamekuwa wakifanya ngono na wanafunzi jambo linalovchangia kutokuwepo kwa umakini kwa wanafunzi hao madarasani, huku wengi wao wakiwapa mimba pasipo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Bw.Wiliard Sengele mkuu wa shule ya msingi Kapunga, alisema hata idadi kubwa ya wanafunzi katika vyumba vya madarasa ni sababu mojawapo inayochangia wanafunzi kutokuwa wasikivu darasani na hawathaminiwi kwani darasa moja linakuwa na zaidi ya wanafunzi 90

Bw.Brown Mwakibete alisema mabadiliko ya mitaala pasipo kuwapa mafunzo yoyote walimu dhidi ya mabadiliko hayo ni chanzo cha wanafunzi kutoelewa, na kuitaka serikali kutofanya mabadiliko pasipo kuwahusisha walimu.

Naye Bw.Abbubakari Chomba alisema baadhi ya watumishi sekta ya elimu ni mzigo kwani hawafahamu wajibu wao, huku wengine wakidiliki kuwa na matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa maendeleo ya elimu (Capitation) kwa kujenga majengo chini ya kiwango, kwa kujali maslahi yao binafsi.

Mbunge wa jimbo la Mbarali Bw. Modestus Kilufi aliwataka watumishi kufuata maadili yao ya kazi, huku wazazi akiwataka kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao ikiwa pamoja na kuwa na ushirikiano baina yao na walimu ili kwa pamoja kufanikisha malezi ya mwanafunzi.

Bw.Kilufi alisema moyo wa kujituma na uzalendo wa kweli wa kulipenda taifa ni nguzo muhimu katika kuinua sekta ya elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kuyafikia malengo waliyojiwekea pasipo kuwakwamisha watoto wa kike kwa kuwapa mimba.

Post a Comment

 
Top