Menu
 

Na Esther Macha, Mbeya
WATANZANIA wametakiwa kuacha kumtafuta mchawi wa hali duni ya maisha yao na kulalamika hali duni ya maisha na badala yake wawe wabunifu,wajitathmini na kufanyakazi kwa bidii na maarifa ili waweze kujipatia kipato na maendeleo ya familia,jamii na taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw.Abbas Kandoro wakati akifungua mkutano wa mashauriano juu ya malengo nane ya melania katika ukumbi wa paradise,jijini Mbeya ambapo wadau kutoka mikoa ya Ruvuma,Rukwa,Njombe,Katavi na Mbeya walishiriki mkutano huo.

Aidha Bw. Kandoro ametoa  maoni yake kuwa endapo kila mtanzania atajituma katika kutafuta maisha na kuzitumia fursa zinazomzunguka,akaacha kuwa mnung’unikaji wa hali ngumu ya maisha huku amekaa kijiweni,akaacha kumtafuta mchawi kwa kila linalomsibu,akawa mchangiaji katika kuhakikisha hali ya utulivu na amani inadumishwa kwa kuheshimu misingi ya utawala bora,kasi ya kuliendeleza taifa itakuwa kubwa.

"Kwa sasa bado tunaongea sana, ‘we are talking a lot,’ninaamini mkusanyiko huu utasaidia sana kufanya tathmini ya pamoja kujuwa tulikotoka,tulipo na tunakokwenda,ninaipongeza serikali kuteuwa Taasisi ya utafiti katika Nyanja za uchumi na jamii (ESRF) ifanye kazi ya kukusanya maoni ya wadau mbalimbali,"alisema .

Alisema utekelezaji wa malengo ya millennia kwa Tanzania unatofautiana kila Mkoa na Wilaya na ametolea mfano kwenye eneo la Ukimwi,Mkoa wa Mbeya una asilimia 9.2 kwa takwimu za mwaka 2008 wakati kitaifa ni asilimia 5.7,kupunguza umaskini kitaifa imetokea asilimia 39 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1990 hadi asilimia 33.6 kwa takwimu za mwaka 2007.

Mkuu huyo wa Mkoa pato la mkazi wa Mbeya kwa siku ni dola 1 hadi 1.5 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2010 ambapo katika elimu ya msingi na Sekondari ukiangalia katika uwiano wa Ke na Me wamevuka lengo kama nchi kwa asilimia 101 na 205 na kwa Mkoa wa Mbeya ni asilimia 102 na 88 ambayo kwa ujumla haijavuka lengo.

Aidha alisema lazima kukiri kuwa bado kuna changamoto katika kutokomeza umaskini wa kipato,njaa,kuboresha afya ya uzazi na huduma za maji salama pamoja na elimu.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema kupitia warsha kutoka katika mikoa yote Tanzania, anao uhakika,ushauri na mapendekeo ya washiriki kuhusu kuamua nini kifanyike kwa siku zijazo baada ya 2015 ni muhimu sana.

Naye Dkt.John Mduma mwezeshaji ambaye ni Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam alisema lengo la mashauriano hayo ni kutoa kichocheo cha mjadala wa wadau mbalimbali,kujenga taswira ya kimataifa ya hali ya baadaye kwa mapendekezo madhubuti,kuhakikisha na kusikika sauti za maskini na wasio sikika,kutambua na kuchambua masuala yatakayoathiri maendeleo,kushawishi mchakato ndani ya serikali kuu ioane na taasisi na matokeo yanayotarajiwa.

Bw.John kajiba ,Mtafiti kutoka taasisi ya utafiti wa mambo ya uchumi na jamii (ESRF-Economic and Social Research Foundation) alisema taasisi hiyo imeombwa kusimamia majadiliano hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya rais tume ya mipango katika kanda saba na hasa katika maeneo ya Serikali za mitaa,Asasi za kiraia,watoto,wazee na wanawake wadogo.

Disemba,4,2012 kumefanyika tukio muhimu na la kihistoria kwa taifa la Tanzania kutokana na kuwa miongoni mwa nchi 50 kati ya 189 zilizochaguliwa kujadili,malengo hayo nane ya millennia katika kanda saba ambazo mahali yalipofanyika katikamabano ni kanda ya Ziwa (Mwanza),kanda ya kaskazini (Arusha),Kanda ya kati(Dodoma),kanda ya nyanda za juu (Mbeya),kanda ya kusini(Mtwara),kanda ya magharibi (Shinyanga) na kanda ya mashariki (Morogoro).

Post a Comment

 
Top