Menu
 

Na Esther Macha, Chunya  
SERIKALI Wilayani Chunya Mkoani Mbeya imewataka watumishi wa serikali kuacha kujihusisha na masuala ya siasa kama watendaji  kwani wanachangia kuleta vurugu ndani ya wilaya badala yake wajikite kutatua kero za wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jana  na Mkuu wa Wilaya ya Chunya ,Bw.Deodatusi Kinawiro wakati akitoa taarifa ya serikali katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri uliopo Wilayani humo.


Bw.Kinawiro alisema  kuwa  kazi kubwa ambayo wanatakiwa kuifanya watumishi wa serikali ni kuangalia hali ya usalama ndani ya wilaya na kutatua kero za wananchi ambazo zinawakabili ,suala la siasa lina wenyewe halipaswi kuwaingilia wahusika.


Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa kumeibuka tatizo kubwa kwa baadhi ya watumishi wa serikali kujihusisha na masuala ya siasa badala ya kazi za wananchi jambo ambalo si zuri kwani watumishi  badala ya kufanya kazi wanazotakiwa wamekuwa wakiacha na kubezi na siasa zaidi jambo ambalo si zuri.


Akizungumzia suala la usalama Bw. Kinawiro alisema kuwa kwasasa wilaya imekuwa shwari  hivyo  ni vema kuendelea kuhamasisha  ulinzi na usalama  ndani ya wilaya hii. “Ni juzi tu kumetokea vurugu za uchaguzi wa kijiji lakini wahusika walikamatwa na mpaka sasa wapo ndani ,kwani wilaya ya chunya haina tabia ya kuwa na vurugu”alisema Mkuu huyo wa wilaya.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Bw.Chakupewa Makelele amesema  kuwa  suala hilo amelipokea atalifanyia kazi kwa kukaa na watumishi  wote wa halmashauri.

Post a Comment

 
Top