Menu
 
Na Shaban Kondo,
 Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la soka nchini TFF imeahidi wadau wa mchezo huo itafanya kazi zake kwa misingi ya haki katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mku wa TFF utakaofanyika jijini Dar es salaam Februari 24.

Mwenyekiti wa kamati hiyo iliyoundwa baada ya waraka wa mabadiliko ya katiba ya TFF kupitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu mwishoni mwa mwaka jana Idd Mtiginjola amesema kamati yake itasimamia misingi ya haki kwa kuvitafsiri vifungu vya katiba pamoja na kanuni za uchaguzi endapo rufaa iltawasilishwa kwao.

Awali katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini TFF Angetille Osiah aliitambulisha kamati hiyo ya rufaa kwa waandishi wa habari na kutoa sababu za kuundwa kwa kamati hiyo itakua ikifanya kazi zake kwa mara ya kwanza baada ya kuingizwa katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu.

Amesema sababu za kuundwa kwa kamati hiyo ni kutaka kutanua wigo wa kupatikana kwa haki pale litakapojitokeza masuala ya utata kama ilivyokua siku za nyumba ambapo kamati ya uchaguzi ilikua inajibebesha majukumu ambayo yalikua si halali kwake.

Baada ya utambulisho huo Angetille Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi  mbalimbali zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, Katiba ya TFF na Katiba ya Shirikisho la soka la Kimataifa la (FIFA).

Mbali ya Iddi Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis Kabwe ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Rufani ya Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.

Post a Comment

 
Top