Menu
 NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Kyela kimesema viongozi wa CHADEMA wanataka kutumia fursa ya uwepo wa mafuta katika tarafa ya Ntebela, kuwachochea wananchi kufanya fujo.

Kufuatia hilo,kiimewatoa hofu wananchi kipo makini, na kitahakikisha kinatoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya utafiti wa mafuta uliofanyika hivi karibuni, na kubaini uwepo wa mafuta katika baadhi ya kata za tarafa hiyo.

Kaimu Katibu wa CCM wilayani humo, Richard Kilumbo, aliyasema hayo mbele ya Mjumbe wa halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Sambwee Shitambala, kwenye maadhimisho ya miaka 36 ya CCM.

Kilumbo alisema:”Juzi na jana wenzetu wa CHADEMA wamekuwa wakiwashawishi wananchi ili tuingie kwenye vurugu kama ilivyotokea hivi karibuni mkoani Mtwara, baada ya kuonekana wilaya yetu inayo mafuta na utafiti umefanyika bado taarifa rasmi kutolewa”.

Aliongeza hivyo CHADEMA wanataka kutumia fursa hiyo ya kuwepo mafuta wilayani Kyela, kuwahamasisha wananchi kufanya vurugu ili machafuko yatokee wilayani humo kitendo ambacho Chama hakiwezi kukubali.

Kaimu Katibu wa CCM wilaya, aliwataka wananchi kuondoa hofu juu ya hilo, kwani mwananchi yeyote ambaye eneo lake analolimiliki likionekana kuwa mkondo huo wa mafuta atalipwa fidia stahili.

Kilumbo alisema wananchi waondoe dhana potofu inayopandikizwa na viongozi wa CHADEMA, kwani CCM itahakikisha hakuna mwananchi anayestahili haki yake halafu akadhurumiwa.

Aliongeza Chama kipo tayari kupambana na CHADEMA na vyama vingine vya upinzani wilayani humo, ambavyo vinajiandaa kufanya kama yale yaliyotokea mkoani Mtwara wananchi kugomea gesi isisafrishwe kwenda Dar es Salaam.

Kilumbo alisema:”Chama kitapita kata zote ambazo mkondo huo wa mafuta umeonekana na kutoa elimu sahihi juu ya uwepo wa mafuta wilayani kwetu…walifanikiwa kuwachochea wananchi wa Mtwara, lakini kwa wilaya ya Kyela wasahau kwani hilo halitawezekana kamwe”.

Post a Comment

 
Top