Menu
 

Mkuu wa wilaya ya Kyela Bi.Margretha Malenga akila kiapo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro.(Picha kutoka Maktaba)
Na Solomoni Mwansele.
MKUU wa wilaya ya Kyela, Magreth Malenga, amesema kazi waliyopewa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, ya kuwaletea maendeleo wananchi inafanyika kwa kasi.

Imeelezwa barabara nyingi, zikiwemo zile za kiwango cha lami na ujenzi wa madaraja likiwemo la Lusungo, zinaendelea vizuri.

Magreth aliyasema hayo jana wakati akielezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa wananchi waliohudhuria maadhimisho ya miaka 36 ya CCM, zilizofanyika kiwilaya  katika viwanja vya siasa, Kyela mjini.

“Ahadi ya Rais Kikwete ya ujenzi wa barabara ya Kikusya kwenda Matema, kwa kiwango cha lami, imeanza kutekelezwa.Vile vile upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Lusungo tayari umekamilika na mara baada ya msimu huu wa mvua kumalizika litaanza kujengwa” alisema na kushangiliwa.

Mkuu wa wilaya aliongeza wakulima wilayani humo, hivi sasa wanaendesha kilimo chenye tija ambacho ndiyo mkombozi wa mkulima, huku ujenzi wa shule za sekondari sambamba na mabweni umekuwa ukiendelea vizuri.

Magreth alisema hivyo ni jukumu la wananchi kumalizia ujenzi wa sekondari hizo pamoja na mabweni, ili serikali nayo iweze kutimiza jukumu lake la kumalizia ujenzi huo na hivyo kuziwezesha kuchukua wanafunzi.

Kwa upande wa sekta ya afya, alisema serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha sekta hiyo inaimarishwa na kuboreshwa zaidi ili wananchi waweze kupata tiba stahili na kwa wakati.

Magreth alisema:”Lakini moja ya changamoto iliyopo ni uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji katika hospitali yetu ya wilaya…hili tunaendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha tunaipatia ufumbuzi kero hii ili hospitali hii iwe kimbilio la wananchi wengi”.

Post a Comment

 
Top