Menu
 

 
Na Solomoni Mwansele.


SHILINGI bilioni mbili zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya halmashauri ya wilaya ya Kyela, kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya kisasa, hazikupelekwa ndani ya halmashauri hiyo.

Imeelezwa kutokana na hali hiyo, halmashauri hiyo iliweza kutumia sh.milioni 100, zilizotokana na vyanzo vyake vya ndani, kuanza ujenzi wa stendi hiyo katika awamu ya kwanza.

Kipija ambaye ni diwani wa kata ya Kyela mjini, aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya miaka 36 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliyofanyika katika viwanja vya Siasa, Kyela mjini.

Mwenyekiti huyo aliongeza katika bajeti ya mwaka huu, pia wametenga kiasi kingine cha shilingi milioni 100, kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa stendi kuu hiyo ya mabasi yaendayo wilayani.

Aliwataka wafanyabiashara wanaomiliki vibanda vilivyojengwa kiholela katika maeneo yanayoizunguka stendi hiyo, waanze mara moja kuyabomoa ili kupisha ujenzi wa stendi mpya.

“Kuna vibanda zaidi ya 50 ambavyo vinatakiwa kubomolewa, ili kupisha ujenzi wa stendi awamu ya pili, hivyo ni vyema kwa wamiliki hawa kuvibomoa wenyewe vibanda vyao ama sivyo halmashauri itavibomoa vyote” alisema Kipija.

Katika hatua nyingine, Kipija alikemea tabia baadhi ya viongozi wa vyama siasa, kikiwemo CHADEMA kuwashawishi wafanyabiashara wanaonunua mazao wilayani kutolipa ushuru.

Alisema hilo ni kosa, kwani kwa kuwajali wafanyabiashara hao, halmashauri hiyo iliwapunguzia ushuru huo kutoka asilimia 5 hadi kufikia asilimia 2.5, lakini bado wanasiasa wamekuwa wakiwashawishi kutolipa.

Alisema wakulima wa wilaya hiyo, ndiyo ambao hawatakiwi kulipia ushuru wa mazao yao, bali wafanyabiashara wanaoenda kununua mazao hayo kwa ajili ya kwenda kuyauza wilaya nyingine ni lazima walipie ushuru.

“Ni vyema watendaji wa vijiji kwa wilaya nzima wazingatie hili, wafanyabiashara wa mazao wanatakiwa kulipia ushuru wa asilimia 2.5 na hili hatutaki kuja kusikia halitekelezwi” alisema Kipija.

Mwenyekiti wa halmashauri alisema wanaendelea na ujenzi wa daraja litakalounganisha kata ya Ndandaro na maeneo mengine yanayoizunguka kata hiyo, ili kuibua fursa za kiuchumi.

Kipija aliongeza vile vile wamekuwa wakiendelea na ujenzi wa barabara mbalimbali, wilayani humo kupitia fedha zinazotengwa katika bajeti ya halmashauri hiyo.

Post a Comment

 
Top