Menu
 

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya imeingia matatani kufuatia wananchi zaidi ya 400, wanaoishi eneo la Masaki Kijiji cha Ichenjezya, Kata ya Vwawa lenye chanzo cha maji kutakiwa kuondoka eneo hilo, na wao kupinga agizo hilo wakidai kulipwa fidia za mali zao kutokana na nyumba za watendaji wa Serikali kuachwa.

Wananchi hao walionekana kukasirishwa na Halmashauri hiyo kufuatia nyumba zao kuwekewa alama nyekundu ya X na bango ya kuwataka kutofanya shughuli zozote za kibinadamu kuanzia Februari 18 mwaka huu ikiwa ni pamoja na kusitisha ujenzi.

 Hata hivyo Diwani wa Kata ya Vwawa Richard Kibona amesema amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wake na suala lao kulipeleka katika Ofisi ya Halmashauri ya wilaya hiyo lakini amekuwa akipigwa danadana na maafisa wa halmashauri hiyo.

Aidha, diwani huyo ameeleza kukerwa na kauli za maafisa hao wa halmashauri kwa kutokuwa wakweli na kumbebesha jukumu nzito la lawama kuwa yeye ndiye asuluhishe mgogoro huo, wakati wakifahamu kuwa suala hilo linatakiwa kujibiwa kitaalamu kutokana na wananchi kumiliki kihalali viwanja na nyumba zao.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake na kueleza kuwa yeye ni Daktari alikataa kata kata kuzungumzia suala hilo kuwa hana mamlaka ya kujibu, akidai kuwa Mkurugenzi ndio mwenye uwezo wa kulizungumzia.

Kutokana na bugudha hiyo kutoka kwa wananchi wake Diwani Kibona alisema wananchi wanamhitaji Mkuu wa Wilaya ya Mbozi ili kupata ufumbuzi wa suala hilo ambalo limewafanya waishi kwa hofu.

Kwa uapande wake Mchungaji Zacharia Mwakasala ambaye pia ni mhanga wa kubomolewa amesema halmashauri ya wilaya hiyo inajichanganya katika maamuzi  kwani eneo hilo walipewa kihalali na kuwekewa mawe(Bicons) na maafisa ardhi kuendelea kulipia kila mwaka na kupewa stakabadhi za wilaya.

Hata hivyo Bwana Philemon Mwaisoloka amesikitishwa na kitendo cha watumishi wa halmashauri hiyo kwa kuweka alama za kubomolewa nyumba zao kwa upendeleo kwani baadhi ya nyumba za vigogo na halmashauri hiyo kutowekewa alama na pia zilizo karibu na maafisa hao zimeachwa bila kuwekwa alamayoyote hali inayojenga hofu ya kuwepo kwa mazingira ya rushwa.

Naye Bi. Happines Mwanijembe ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa baadhi ya nyumba kama vile ya Afisa mipango, Afisa ardhi, Afisa mazingira, Afisa misitu, Afisa utumishi, Askari wa jeshi la Polisi, Afisa wa benki ya NMB na Meneja wa CRDB zimeachwa huku maafisa wanaondesha zoezi la kuweka alama wakijinufaisha kwa pesa kutokana na baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo kutaka wawalinde.

Hata hivyo juhudi za kumpata Mkuu wa wilaya Ndugu Kadege hiyo ziligonga ukuta baada ya kuwa nje ya Ofisi kikazi ambapo Afisa mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mpandachombo, kukiri kupokea malalamiko ya wananchi hao na kwamba suala hilo atamfikishia ili atolee maamuzi.

Post a Comment

 
Top