Menu
 

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya..
 MBUNGE wa Mbeya vijijini (CCM) Lackson Mwanjali ameingia lawamani baada ya wanachi wa Kitongoji cha Italazya kata ya Ilembo Wilaya ya Mbeya kumtuhumu Mbunge huyo kwa kutoa ahadi hewa ambayo ameshindwa kuitekeleza.
 
 
Mbunge huyo aliwaagiza wananchi hao kujenga shule ya msingi katika kitongoji chao kutokana na umbali wa shule nyingine inayosababisha watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule.
 
 
Mbunge huyo aliwaambia wananchi hao kujenga majengo ya vyumba vya madarasa hadi kufikia usawa wa mtambaapanya(renta) ambapo yeye atamalizia kupitia mfuko wa jimbo.
 
 
Hata hivyo kufuatia ahadi hiyo hali hiyo imekuwa kinyume na matarajio ya wananchi hao ambao wamesema tangu atoe agizo hilo mbunge huyo hajawahi kurudi kijijini hapo wala kutekeleza ahadi hiyo.
 
 
Wananchi hao walisema kufuatia hali hiyo walilazimika kumfuata mara kadhaa mbunge huyo ofisini kwake ili wamkumbushe kuhusu ahadi yake baada ya wao kukamilisha usawa waliopangiwa na mbunge wao lakini waliishia kuahidiwa tu.
 
 
Aidha wananchi hao walisema Mbunge huyo amewavunja nguvu baada ya majengo waliojenga kuanza kubomoka hali iliyosababisha kukatishwa tamaa na utekelezaji wa ahadi hiyo.
 
 
"Tumejaribu kumfuata mara kadhaa ofisini kwake kuhusu kutekeleza ahadi yake hiyo lakini anaendelea kutuahidi hali inayoonesha kutudanganya tu" alisema Adson Kinga mjumbe wa Serikali ya Kitongoji.
 
 
Alisema juhudi kubwa iliyofanywa na wananchi katika kujenga majengo hayo ambayo walisema ilikuwa ni ukombozi wa watoto wa kutotembea umbali mrefu lakini juhudi hizo zimeyeyuka baada ya jengo kuanguka kutokana na kutoendelezwa.
 
 
" Ingekuwa ni kilimo tungekuwa tuko kwenye mavuno makubwa kutokana na nguvu tuliyoitumia kujenga madarasa hayo lakini tunasikitishwa na mbunge kutusahau wakati sisi ndiyo tuliomchagua" alisema Furaha Mwafowela mkazi wa Kitongoji hicho.
 
 
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hiyo hakupokea simu zake za kiganjani ambazo ziliita mda mrefu bila kupokelewa.

Post a Comment

 
Top